Kesi ya Mbowe: “Polisi Walinichukulia Sh 12,500, Nikabakiwa na Sh 200”



ALIYEWAHI kuwa Mwanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2000 hadi 2014 na baadaye kuacha siasa na kujiunga na Chuo cha Usafirishaji (DIT), Lukola Kahumbi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Askari Polisi walimwambia ajiongeze kisha wakampekua na kumchukulia Sh. 12,500 na kumuachia Sh. 200.

 

Mwanafunzi huyo ni shahidi wa 13 katika kesi ya Uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa CHADEMA ambapo ameeleza kuwa hali hiyo ilimpelekea kutembea kwa miguu kutoka kituoni hapo hadi chuoni.

 

Kahumbi ni shahidi wa Utetezi katika kesi hiyo, ameyaeleza hayo wakati akiongozwa na Wakili Peter Kibatala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

 

Akitoa ushahidi wake amedai kuwa mwaka 2018 alikuwa akisoma Chuo cha DIT akichukua Shahada ya Kwanza ya Uhandisi wa Umeme na Mawasiliano, ambapo kwa sasa anaishi Mbezi Kimara.

 

Wakili Kibatala amemuuliza shahidi huyo kama aliwahi kuwa Mwanachama wa chama chochote ambapo alimjibu alikuwa Kada wa CCM mwaka 2000 hadi 2014 ambapo pia aliingia Umoja wa Vijana lakini baadaye akaachana na siasa na kujiunga na Chama cha usafirishaji cha Taifa.

 

Alipoulizwa Februari 16, 2018 alikuwa wapi alijibu kuwa alikuwa akitokea chuoni kuelekea kwa shangazi yake Studio Kinondoni kwa kutumia Daladala.

 

Ameeleza kuwa mara baada ya kushuka akiwa Kituo cha Daladala akielekea kwa Shangazi yake ambapo ni nyumba ya nne kutokea hapo aliona magari ya Polisi mengi.

 

Amedai kuwa aliwaona Askari Polisi wanashuka kwa kuruka kutoka katika magari hayo jambo ambalo liliibua taharuki na kufanya watu wakimbie akiwemo yeye.

 

Alifafanua kuwa walikamatwa watu mbalimbali wakiwemo wauza vitanda vya chuma wakawekwa katika gari(Difenda) na yeye aliwekwa chini ya siti na wengine wakapandishwa juu na kuchanganywa wanawake na wanaume na kupelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay.

 

Shahidi huyo, amedai kuwa baada ya kufikishwa Kituoni waliwaweka eneo la nje ambapo Askari walitoka ndani na kuanza kuwapiga mikanda, kisha Askari mmoja alitoka na kumpa mmoja wao apige ngoma na wao waanze kuimba.

 

“Askari walichukua Elfu 12 na 500 na wakaniachia Mia 200 na wakanambia niondoke nisigeuke nyuma,”

 

Baada ya kuhojiwa na Kibatala, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alimuuliza shahidi huyo kwamba ni sahihi alipowaona Askari alikimbia na kukamatwa na alipelekwa Oysterbay Polisi, alijibu ni sahihi.

 

Pia Nchimbi alimuuliza shahidi huyo kama ni sahihi ushahidi wake haukueleza chochote kuhusu risasi, shahidi alijibu ni sahihi.

 

Pia shahidi huyo aliulizwa akiwa Kituo cha Polisi alisikia mazungumzo yoyote ambapo alijibu ndio aliyasikia ikiwemo watu kushangazwa na jinsi walivyokamatwa pamoja na mazungumzo ya Askari waliokuwa wakisema Askari wa Depo wameua mtu.

 

Pia shahidi huyo aliulizwa Askari waliomchukulia Hela alikutana nao chooni? alijibu alikutana nao kwenye Muembe wakati akielekea chooni.

 

Washtakikiwa katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Dk.Vincent Mashinji.

 

Washitakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam.



Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad