Kijana Amkata Kata Mapanga Baba yake Mzazi Kisa ni Maskini....
0
January 24, 2020
MADAI ya kuwa yeye ni masikini ni sababu iliyomtosha Chacha Makonge ‘23’ kutaka kumuua kwa kumkata mapanga sehemu mbalimbali mwilini baba yake mzazi Makonge Mwita (90).
Chanzo cha habari kinaeleza kuwa mara kadhaa Chacha alidaiwa kumweleza baba yake kuwa amechoka kutaabika na hivyo kumuomba mzazi wake huyo mwenye wake 12 ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Masangura Kata ya Nyamoko ampatie sehemu ya mali ili aweze kuishi maisha bora.
Hata hivyo, chanzo chetu kinaeleza kuwa mzee Makonge hakuweza kumpatia mali mwanaye hadi siku ambayo aliuza ng’ombe kadhaa na kujipatia kiasi cha shilingi milioni tatu ambazo ndizo zilizozua tukio hilo la kinyama.
ILIKUWAJE SIKU YA TUKIO?
Januari 9, mwaka huu mzee Makonge mwenye kaya nyingi na mifugo ya kutosha Wilaya za Tarime na Serengeti, aliuza ng’ombe (idadi haikutajwa) na kupata fedha kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ambapo Chacha aliyekuwa anaishi naye, alianza kuzipigia hesabu ya kuzitwaa.
Akifafanua kwa kina kuhusu tukio hilo, Joseph Makonge (33) ambaye ni mtoto mkubwa wa mzee huyo, alimwambia mwandishi wetu kuwa: “Usiku wa saa 7 tulisikia yowe ikipigwa nyumbani kwa mzee maana mimi nilishajitenga, nikachukua zana zangu za kujihami. Nikatoka kwenda kumsaidia baba huku nikiongozana na majirani,” alisema.
Aliongeza kuwa walipofika walikuta mlango wa nyumba ya mama yake mdogo ambaye alikuwa anapiga kelele kuomba mumewe asaidiwe asiuawe uko wazi.“Kumulika ndani tulimuona baba akiwa amelala chini, akiwa ametapakaa damu kichwani na mwilini. Mama mdogo akasema watu wawili walivunja mlango na mmoja wao ni Chacha ambaye ni mdogo wangu, nilishikwa na uchungu sana.
“Mama alisema alimuona akimkata mapanga baba huku akimlazimisha ampe fedha, mzee alipochelewa kutoa fedha ndipo akawa anamshambulia kwa mapanga, baba akaona anaweza kuuawa ndipo akaamua kumpatia hizo shilingi milioni tatu alizopata kwa kuuza ng’ombe. “Chacha mdogo wangu siku hiyo mpaka jioni alikuwepo nyumbani maana ndiye anayeishi na mzee, lakini baada ya tukio hilo hajaonekana tena,” alisema.
SABABU ZA KUFANYA HIVYO
Joseph aliongeza kuwa mdogo wake alikuwa na tuhuma za kumuibia baba yao mifugo na kuuza; tatizo ambalo lilikuwa limesharipotiwa kwenye vyombo vya serikali. Sababu za kufanya matukio hayo yote likiwemo hilo la kumcharanga mapanga baba yake ni kujipatia mali.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa watuhumiwa wanasakwa na polisi hivyo jamii inatakiwa kuwafichua mahali popote walipojificha. “Haya ni matokeo ya watu wasiofanya kazi; wanavizia kuwamaliza wazee wao kama huyo ili wapate mali kwa njia ya mkato,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Hata hivyo, habari kutoka polisi zinadai kuwa kuna kijana mwingine wa mzee huyo ana kesi mahakamani ya kumuibia baba yake mifugo na kwamba naye anasakwa kwa tuhuma za kuhusika katika kumshambulia mzee Makonge ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Nyerere akipatiwa matibabu
Tags