Ugunduzi wa mfumo mpya wa kinga unaweza kutumika kutibu aina zote za saratani, wanasema wanasayansi.
Kundi hilo kutoka chuo kikuu cha Cardiff liligundua mtindo wa kutibu saratani ya tezi dume, ile ya matiti ya mapafu na aina nyengine za saratani katika vipimo vya maabara.
Matokeo yake yaliochapishwa katika jaradi la kinga asli ,hayajajaribiwa miongoni mwa wagonjwa lakini wanasayansi hao wanasema yana uwezo mkubwa.
Wataalam wanasema kwamba ijapokuwa kazi hiyo ilikuwa hatua za kwanza ilikuwa inafurahisha.
Wanasayansi hao walikuwa wakitafuta njia ambazo hazijagunduliwa kuhusu jinsi mfumo wetu wa kinga unavyoshambulia uvimbe unaosababisha saratani.
Kile walichogundua ni seli aina T ndani ya damu. Hii ni seli katika kinga ambayo inaweza kupima iwapo kuna tishio mwilini ambalo linafaa kuondolewa.
Tofauti yake ni kwamba seli hiyo inaweza kushambulia aina tofauti za saratani.
Kuna fursa hapa ya kutibu kila mgonjwa, mtafiti profesa Andrew Sewell aliambia BBC.
Aliongozea: Awali hakuna aliyeamini kwamba hili linaweza kufanyika. Inatoa fursa ya tiba moja kutibu saratani zote, seli moja aina ya T inayoweza kuharibu aina tofauti ya saratani miongoni mwa waathiriwa.
Kundi hilo la Cardif liligundua seli aina ya T na receptor yake ambayo inaweza kugundua na kuuwa idadi kubwa ya seli za saratani katika maabara ikiwemo katika mapafu, ngozi, damu, koloni, matiti, tezi dume, mayai na shingo ya uzazi.
Mfano maarufu ni ule wa CAR-T - dawa ya jeni ilioundwa kushinikiza seli ya T kushambulia ama kuharibu seli za saratani mwilini
CAR-T inaweza kuwa na matokeo ya kushangaza ambayo huwafanya baadhi ya wagonjwa kuwa wagonjwa zaidi na kusalimu amri.
Hatahivyo mtazamo huo ni wa aina yake na unafanya kazi katika aina chache za saratani ambapo lengo kuu ni kuzifunza kutafuta seli za saratani.
Na imeshindwa kuwa na mafanikio yoyote katika saratani kama vile zile zinazosababisha uvimbe badala ya zile za damu kama vile saratani ya damu.
Watafiti wanasema kwamba seli aina ya T inaweza kusababisha tiba ya saratani duniani.
Lengo ni kwamba sampuli za damu zitachukuliwa kutoka kwa mgonjwa anayeugua saratani. Seli zake aina ya T zitatolewa na baadaye kuwekwa jeni ili kuzifanya kuweza kubaini seli za saratani.
Seli hizo zitakuzwa ili kuongezeka kwa wingi katika maabara na baadaye kurudishwa katika mwili wa mwanadamu .
Hatahivyo utafiti huo umefanyiwa majaribio katika wanyama pekee na katika seli za maabara, na vipimo salama vitahitajika kufanywa kabla ya matumizi ya mwanadamu.
Lucia Mori na Gennaro De Libero, kutoka chuo kikuu cha Basel nchini Switzerland, wanasema kwamba utafiti huo una fursa kubwa lakini ni mapema mno kusema kwamba utafanikiwa kufanyakazi katika saratani zote.
''Tunafurahi sana kuhusu kazi ya seli hiyo ya kinga na matumizi ya TCRs katika tiba ya uvimbe'' ,alisema.
Daniel Davis, ambaye ni profesa wa kinga katika chuo kikuu cha Manchester, alisema: Huu ni utafiti wa msingi na hauko karibu kupata tiba ya saratani.
''Ni wazi kwamba ni ugunduzi mzuri, utakaoendeleza maarifa yetu ya kimsingi kuhusu mfumo wa kinga na uwezekano wa dawa mpya za baadaye."