Kisa Simba, Bilionea Aimwagia Yanga Mamilioni Dar



SARE ya mabao 2-2 waliyoipata Yanga walipocheza na Simba katika mchezo wa watani wa jadi, imewafanya wapate Sh milioni 50 kutoka kwa wadhamini wao, Kampuni ya GSM inayomilikiwa na bilionea Ghalib Mohamed, lakini kama wangeshinda GSM ingewazawadia Sh milioni 200.

 

Timu hizo zilivaana Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa, Simba wakitangulia kupata mabao kupitia kwa Meddie Meddie na Deo Kanda huku Yanga wakichomoa yote kupitia kwa Mapinduzi Balama na Issa Mohamed ‘Banka’.

 

Yanga imekuwa na kawaida ya kupewa ahadi ya Sh milioni 10 kila inapopata ushindi kutoka kwa GSM ambayo imekuwa ikitoa kama posho ili kuwapa morali wachezaji wake wapate ushindi.

 

Kwa mujibu taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo kabla ya mchezo huo kuanza, mabosi wa GSM chini ya Mkurugenzi wa Uwekezaji wa kampuni hiyo, Hersi Said walitoa ahadi hiyo ya Sh 200mil kama wangeibuka na ushindi kwa ajili ya kuwapa wachezaji morali.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa ahadi hiyo walipewa muda mchache kabla ya kutoka Regency Hotel, Mikocheni Dar ilipoweka kambi timu hiyo ikijiandaa na mchezo huo.

 

Aliongeza kuwa, baada ya mchezo kuisha kwa sare GSM wamewapa Sh milioni 50 kama pongezi kwa kiwango chao walichokionyesha katika mchezo huo kwa kucheza soka safi huku wakisawazisha mabao yote mawili yaliyofungwa na Mapinduzi Balama na Issa Mohamed ‘Banka’.

 

“Ilitakiwa kila mchezaji aondoke na Sh 7mil kama tungefanikiwa kuwafunga wapinzani wetu Simba, kwani kabla ya pambano hilo GSM tulifanya nao kikao na kutuahidi Sh 200mil tukiwa kambini kama tungefanikiwa kuwafunga Simba.

 

“Ndiyo maana uliona morali ya wachezaji kuwa kubwa katika mchezo huo, hasa katika kipindi cha pili mara baada ya timu iliporudi uwanjani kutokana na maelekezo waliyoyapata kutoka kwa kocha Mkwasa (Charles) na Niyonzima (Haruna) ambaye alionekana kuwapa mbinu na kuwaondoa hofu wachezaji chipukizi kama Makame (Abdulaziz) kutulia na kucheza kwa kujiamini.

 

“Lakini, licha ya kuzikosa Sh 200mil hizo wachezaji walipewa 50mil kama sehemu ya pongezi kutokana na kiwango kikubwa walichokionyesha wachezaji wetu hasa katika kipindi cha pili ambacho tuliwashambulia kwa dakika zote na kufanikiwa kusawazisha mabao hayo yote mawili.

 

“GSM wamefurahishwa na kiwango kikubwa cha wachezaji wetu ambacho wamekionyesha wakiamini kuwa kama yasingekuwa maamuzi mabaya ya waamuzi, basi wangepata ushindi,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa nahodha msaidizi wa timu hiyo, Juma Abdul kuzungumzia hilo alisema: “Ni kweli GSM walituahidi pesa nyingi ambazo kama tungewafunga Simba na hiyo imekuwa kawaida kwa kampuni hii kutupa motisha wachezaji siku moja kabla ya mechi.

 

“Licha ya kukosa hizo nyingi tulizozikosa, lakini tunashukuru wametupatia kiasi fulani cha pesa kama sehemu ya pongezi kwetu wachezaji, tunashukuru, kwetu wachezaji inatuhamasisha kuipambania timu.”


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad