Na Said Said Nguya
Desemba 23 mwaka jana, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ali alianza likizo ya mwaka kwa siku Kumi, ambapo mpaka Januari 03 mwaka huu alikuwa nyumbani kwao Bukoba vijijini, mkoani Kagera.
Ameshuhudiwa akitumia muda mwingi wa mapumziko yake, katika shughuli mbalimbali za kijamii na kisiasa, akitoa ufafanuzi na maelekezo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha zaidi Chama hicho.
Kupitia mkutano wa ndani wa wenyeviti wa mitaa na vijiji wilayani Bukoba, Dkt. Bashiru alitoa msimamo wa chama katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, mwishoni mwa mwaka huu, kwamba CCM kitafanya siasa safi, kikiheshimu maamuzi ya Umma kama ambavyo kimekuwa
kikifanya kwenye chaguzi nyingine.
Dkt. Bashiru pia alitumia mkutano huo kutoa ufafanuzi kuhusu hoja mbalimbali za vyama vya upinzani, ikiwamo ile ya madai ya tume huru ya uchaguzi.
Alielezea hoja hiyo kuwa haina mashiko kwani jukumu kuu la tume ya uchaguzi, ni kusimamia uchaguzi si vinginevyo kwahiyo, chama kisipokuwa na wapiga kura, tume ya uchaguzi haiwezi kukisaidia kupata ushindi.
“CCM kinaendelea kutafuta wapiga kura kwa kusomesha wanafunzi bure, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kuboresha na kuimarisha huduma za kijamii ikiwamo kujenga vituo vya afya, barabara sasa, huduma za maji na umeme…, sasa wao waseme wanatumia njia gani kupata
wapiga kura na wanawafanyia nini wapigakura wao?,” alisema Dkt. Bashiru.
Alitamba kuwa mpaka sasa CCM ndicho pekee kilichoweka wazi msimamo wake wa kupinga udharirishwaji na ubaguzi wa wanawake, katika ngazi tofauti za uongozi.
“Mara nyingi imeshuhudiwa wanawake kabla ya kugombea wakiitwa majembe, kwenye vyama Fulani vya siasa lakini wakichukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi za uongozi, wanachimbwa na kuwekewa kashfa nyingi, wanatishwa na hata kufanyiwa mambo ya hovyo, awamu hii CCM
hakitakubali wamawake wadharirishwe,” alisema.
Akizungumzia mchakato wa kupata wagombea ndani ya chama hicho, Dkt. Bashiru, alikemea tabia ya baadhi ya wanaCCM kuabudu majina ya watu, kwa imani kuwa majina ya watu hao yasipopitishwa kugombea chama haiwezi kushinda.
Hatua hiyo imeibua ari mpya miongoni mwa wanaCCM wa maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Jimbo la Bukoba mjini, ambalo ni sawa na Jimbo lisilo na mwakilishi kufuatia Mbunge wake, Alfred Lwakatare kutokuwa karibu na wananchi kwa muda mrefu, huku chama chake cha Chadema kikikosa
mvuto kisiasa jimboni huo.
Alipotembelea na kukagua ujenzi wa ofisi ya chama hiko kwenye Kata ya Bwanjai, wilayani Misenyi Dkt. Bashiru alitaka wananchi kupuuza baadhi ya sera na kauli za viongozi wa vyama vya siasa, zinazolenga kurejesha nyuma maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Viongozi tunaongoza mapambano ya kujikomboa kiuchumi, kila mtu anahitajika kuhimiza kufanya kazi kwa bidii, kwamfano CCM tuna kauli mbalimbali za kuhimiza hilo ikiwamo, Hapa Kazi tu, Kazi na Maendeleo, Uhuru na Kazi pamoja na ile ya Kazi ni Utu, ajabu ni kwamba kuna vyama vinahubiri kazi na starehe…, hapa ndipo mnapoweza kuona tofauti kati ya chama kiongozi na vyama vya uchaguzi,” alisema Dkt. Bashiru.
Kauli za aina hiyo alizitafsiri kuwa kauli za kipumbavu, akaomba watanzania kuzidharau kwasababu zinatolewa na viongozi wasiokuwa na ni njema na taifa, wenye hulka ya kulaghai umma kwa kutumia siasa nyepesi.
Nao viongozi wa chama na serikali, walipewa maagizo anuai ikiwamo agizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya, kuhakikisha wafanyakazi, wahudumu na mafundi kwenye miradi yote inayotekelezwa na serikali, ambayo imeishapelekewa fedha na serikali kuu wanalipwe haki zao kwa wakati.
Agizo hilo lilifuatia hatua yake ya kukagua mradi wa ujenzi hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, ambao pamoja na kuwa katika hatua za mwisho, alipokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wa mradi huo kwamba hawakuwa wamelipwa fedha zao.
Dkt. Bashiru pia alihimiza utekelezwaji wa azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa, linalotaka kamati za siasa za mikoa na wilaya, kuwasilisha maoni yao kabla ya Januari15 mwaka huu, kwa ajili ya kukamilisha Ilani ya uchaguzi na mwelekeo wa Sera za CCM 2020-2030.
Alivitaka na vyama vya upinzani pamoja na makundi mengine ya kijamii, kutoa maoni yao ili yaingizwe kwenye ilani ya CCM kwasababu kutokana na kasi ya uongozi na ubora wa huduma zinazotolewa na serikali inayoongozwa na chama hicho, hakuna ubishi kwamba kitashinda katika
uchaguzi mkuu ujao, baadaye mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa, katika Kikao cha Halmashauri kuu ya Taifa iliyofanyika Desemba, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, alitoa hotuba ya ufunguzi wa semina ya Wajumbe hao iliyoonekana kusisimua wajumbe kwa kugusa maeneo yote muhimu ya maendeleo, na Makaku mwenyekiti wa CCM Zanzibara na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein alitoa hotuba ya kufunga, ambazo hotuba zote mbili ziliamuliwa ziwe ndio miongozo katika uandishi wa Ilani na Mwelekeo wa sera wa Chama hiko kongwe barani Afrika.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya kuzindua makazi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amoni Mpanju, kwenye Kijiji cha Nyakibimbili, aliasa jamii kusaidia watu wenye ulemavu ili waweze kung’amua fursa, kupitia vipawa vyao kama ilivyofavyika kwa Mpanju.
“Inatakiwa tuwapende zaidi watu ambao kwa maumbile yao hawawezi kutenda baadhi ya mambo bila msaada, lakini wanavipawa vya kusaidia jamii yao na nchi kwa ujumla, Amoni ni miongoni mwa watu wanaotusikia lakini hawatuoni…, namfahamu vizuri, ni miongoni mwa vijana wachapa
kazi zaidi hata ya wanaoona, majukumu aliyonayo hajapewa kwa upendeleo bali anayamudu sawasawa,” alisema Dkt. Bashiru.
Pia alihimiza zaidi upendo kwa watoto, akisema CCM kimeonesha njia kwa kuweka utaratibu wa elimu bila malipo, kwamba watoto wengi wamepata fursa ya kupata elimu tofauti na awali.
Naye Mpanju, akizungumza wakati akimkaribisha Dkt. Bashiru alielezea ugumu aliyokabiliana nao katika maidha yake, ikiwamo kufiwa na wazazi wake wote wawili akiwa katika umri mdogo, hali iliyosababisha asomeshwe na watu ambao baadhi hakuwa akiwafahamu.
Pamoja na watu hao, alishukuru itikadi ya Ujamaa akisema bila itikadi hiyo iliyojenga na kueneza udugu na ujamaa miongoni mwa watanzania, ana uhakika asingesoma.
Mwandishi ni Mchambuzi wa siasa na maendeleo nchini.