Mahakama imempa pole Mwandishi wa Habari za uchunguzi, Erick Kabendela kwa kufiwa na Mama yake mzazi, Verdiana Mujwahuzi huku ikiyapinga maombi yake ya kutaka kwenda kushiriki Ibada ya mazishi ya mama yake.
Hiyo imebainika leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati Kabendera anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha alipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kesi yake kutajwa.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amemueleza Hakimu Mkazi, Janeth Mtega kwamba Jamhuri inampa pole Kabendera kwa kufiwa na Mama yake mzazi.
Wankyo amedai kuwa maombi ya Kabendela kupitia mawakili wake yamewasilishwa wakati ambao si sahihi kwa sababu mahakama haina mamlaka na pia Mkurugenzi wa Mashitaka hajaipa kibali ya kusikiliza kesi hiyo.
Kukataliwa kwa Kabendera kushiriki mazishi ya Mama yake, kumeibuka kutokana na maombi aliyoyatoa Kabendera kupitia Mawakili wake akiwemo Jebra Kambole.
Wakili Kambole amedai wanaiomba mahakama hiyo imruhusu Kabendera akashiriki Ibada ya Mazishi ya Mama yake mzazi katika Kanisa la Roman Katoliki lilipo Changombe majira ya mchana.
Kambole ameieleza mahakama kuwa suala la kushiriki sala ya mwisho ya msiba ni haki ya Binadamu, suala la faragha.
“Kushindwa kuudhuria maziko ya Mama yake tutakuwa tumemuadhibu adhabu kubwa tena kwa kuangalia uhusiano wa mshitakiwa na mama yake mzazi kwani alikuwa akimuuguza na ni vizuri akatoa heshima ya mwisho,”ameeleza.
Wakili Jebra amedai kuwa ni muhimu kwa Kabendera kushiriki kwa sababu Mama mzazi ni mmoja, akifa anaagwa mara moja.
Baada ya kutoa hoja hizo, Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi saa 8:45 mchana kwa ajili ya kutoa uamuzi kama Kabendera ashiriki Ibada ya mazishi ya Mama yake mzazi ama lah.
Mama Kabendera alifariki dunia Desemba 31, 2019 ikiwa ni wiki kadhaa baada ya kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amsamehe mtoto wake.
Kabendera anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu ikiwemo la utakatishaji wa Sh.Mil 173.