Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Selikali imezipiga marufuku taasisi zote za Umma nchini kujenga mifumo ya fedha ya kieletroniki bila ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
Agizo hilo limetolewa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, wakati akizundua Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya Kielektroniki (GePG) toleo la simu za mkononi (GePG App), hafla iliyowakutanisha Wizara ya Fedha na Mipango na Idara, Wakala, Taasisi, Bodi, Mashirika ya Umma yaliyo katika Kanda ya Kati.
Bw. James alisema kuwa Taasisi zote za Umma nchini zinatakiwa kutekeleza matakwa ya Waraka namba tano (5) wa Hazina unaozitaka taasisi zote kuhakikisha zinapata ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango na Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) kabla ya kufanya ununuzi, uandaaji, usimikaji na utumiaji wa Mfumo wowote wa kielektroniki wa usimamizi wa Fedha za Umma.
“Imebainika kuwa kuna baadhi ya taasisi za umma ambazo zinakiuka maelekezo hayo ya Serikali kwa sababu wanazozijua wao, nitumie fursa hii kutoa onyo kwa taasisi hizo kutoendelea na vitendo hivyo kwa sababu ni ukiukwaji wa maelekezo”, alisema Bw. James.
Akizungumzia kuhusu GePG App, Bw. James alisema kuwa, uboreshaji wa Mifumo ya Kielektroniki inayoandaa Ankara itawezesha kukusanya fedha kwa wakati na kutoa huduma bora kwa Umma.
“Baadhi ya faida za Matumizi ya Mfumo huo ni kuongezeka kwa uwazi na udhibiti katika ukusanyaji wa fedha za umma, kupata taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu makusanyo na kuwa na viwango na utaratibu unaofanana katika ukusanyaji wa fedha za umma kwa taasisi zote za umma”, alisema Bw. James.
Alisema faida nyingine ni pamoja na kuchochea ubunifu katika ukusanyaji wa pesa za Serikali na sekta ya fedha kwa ujumla kwa kuweka mazingira rafiki na ya usawa kwa wakusanyaji, kutoa huduma bora na rahisi ya malipo ya fedha za umma hivyo kuchochea ongezeko la makusanyo na kufika haraka katika akaunti kuu za makusanyo za taasisi.
“Kwa kutofanya usuluhishi wa miamala kwa wakati kunaweza kusababisha upotevu wa fedha nyingi za Umma na pia kuwa na taarifa za fedha zisizo sahihi, hivyo nawaagiza nyote kuhakikisha mnafanya usuluhishi wa miamala inayopitia Mfumo wa GePG kwa usahihi na kwa wakati, na kufanyia kazi kwa wakati changamoto mbalimbali zitokanazo na matokeo ya usuluhishi wa Miamala husika”, alisisitiza Bw. James.
Aidha alimpongeza Mkurugenzi wa Mifumo ya Usimamizi wa Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Sausi pamoja na timu yake ya wataalam wabobezi kwa kutengeneza Mfumo wa Kieletroniki wa Kukusanya Mapato ya Serikali (GePG) sambamba na toleo la simu za mkononi (GePG App) ambao umerahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali pamoja na kuwawezesha wadau kupata huduma kwa wakati.
Aliahidi kuwa Wizara yake itaendelea kuiwezesha Idara hiyo ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kubuni mifumo kama hiyo kwa faida ya Serikali na wananchi kwa ujumla.
Aidha, Bw. James ambaye pia ndiye Mlipaji Mkuu wa Serikali, alisema kuwa Wizara kupitia Idara ya Mifumo ya Usimamizi wa Fedha inaandaa mfumo mwingine utakaotumika kwa ajili ya matumizi ya Serikali ujulikanao kwa kifupi kama MUCE.
“Mfumo huu umeshaanza kufanyiwa majaribio kwenye taasisi chache za umma na baadae utasambazwa kwenye taasisi zote na kwamba Mfumo huu utakuwa mwarobaini wa matumizi yasiyo sahihi ya fedha za Umma”, aliongeza Bw. James.
Alisema Mfumo huo utakuwa suluhisho la matumizi yasiyofaa ya umma na kuongeza kuwa watendaji wengi Serikalini hawataufurahia mfumo huo lakini hilo haliihusu Serikali. Watajua wenyewe! Alisema huku washiriki wakiangua kicheko ukumbini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mifumo ya Fedha, wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Sausi, alisema kuwa kabla ya kuwa na Mfumo wa Malipo kwa njia ya Kielektroniki (GePG) ilikua inafanyika miamala 10 kwa siku na baada ya mfumo huo inafanyika miamala milioni moja kwa siku.
Alisema kuwa miongoni mwa mafanikio ni kuongezeka kwa Taasisi zinazotumia Mfumo wa GePG, kutoka taasisi 300 muda mfupi uliopita hadi kufikia taasisi 620 hivi sasa.
Bw. Sausi alisema kuwa Mfumo wa GePG kwa njia ya mtandao wa simu za mkononi uliozinduliwa utasaidia watumiaji kupata huduma mbalimbali kama vile kununua umeme, kulipia Ankara mbalimbali zikiwemo za makosa ya usalama barabarani, maji na nyingine nyingi ndani ya sekunde 30.
Ametoa wito kwa wananchi wanaotumia simu janja (android au IPA App) kupakua application hiyo kupitia play store au App Store na kutafuta neno GePG Tanzania tayari kwa matumizi yao ambayo amesema wananchi watafurahia huduma hiyo.
Naye Mwakilishi wa Benki katika Mkutano huo, Bi Domina Tarimo na Mwakilishi wa kampuni za Simu, Bw. Alafat Ibrahim, walisema kuwa Mfumo wa GePG umezisaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha kazi zao, na kuboresha huduma kwa wateja wao na wameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango na Serikali kwa ujumla kwa jitihada zake za kuhakikisha kuna mifumo imara ya fedha inayoongeza uwazi na uwajibikaji.