Mashirika kadhaa makubwa ya ndege duniani yamesema hii leo kwamba yanabadilisha njia za safari za ndege ili kuliepuka anga la Iraq na Iran baada ya Shirika la Marekani la usafiri wa angani, FAA kuzizuia ndege za taifa hilo kutumia anga hiyo kufuatia shambulizi la makombora lililofanywa na Iran kwenye vikosi vya Marekani nchini Iraq.
FAA imesema imetoa zuio la anga ambalo pia linajumuisha anga za Ghuba na Oman na eneo la bahari kati ya Iran na Saudi Arabia kutokana na kile ilichotaja kuwa ni kuongezeka kwa shughuli za kijeshi na wasiwasi wa kisiasa Mashariki ya Kati hali inayotishia shughuli za anga za Marekani.
Shirika la ndege la Emirates la Dubai limeahirisha safari za Baghdad hii leo na kusema huenda likafanya mabadiliko zaidi ya safari zake. Mashirika mengine yaliyoashiria kuondoa safari zake ni ya Singapore, Malaysia, China na Austarlia.