IKIWA ni saa chache baada ya taarifa kutolewa kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini Uingereza kuwa straika wa timu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji na nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Ally Samatta, amejiunga na Klabu ya Aston Villa, mashabiki wa Genk (kupitia ukurasa rasmi wa mashabiki wa timu hiyo kwenye Instagram) wameonyesha kuhuzunishwa na kuondoka kwa mchezaji huyo huku wakimtakia kila la heri aendako.
“Ulikuja kama kijana wa kawaida, lakini sasa unaondoka kwa heshima kupitia lango kuu ukiwa kama gwiji. Tunalia kwa kuwa unatuacha lakini tunajivuna na kuona fahari kwa kuwa tumekushuhudia ukiwa umevaa jezi yetu kwa kipindi cha miaka minne. Wewe ni mmoja kati ya watu wakubwa na wa maana sana katika historia ya Genk,” wamesema mashabiki hao.
Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza, imemsajili Samatta kwa ada ya Paundi milioni 9 na atatambulishwa rasmi kwenye klabu hiyo leo baada ya kufanyiwa vipimo vya afya.
Baba mzazi wa Samatta, Ally Pazi Samatta, amesema, “Amenipigia simu kunitaarifu kwamba yuko safarini kwenda Uingereza kufanyiwa vipimo na baadaye kukamilisha mipango mingine. Namuombea Mungu amfanyie wepesi katika hatua aliyofikia ili atimize ndoto zake za kucheza Ligi Kuu ya England.”
Samatta anaruka kutoka Düsseldorf Ujerumani ambako Genk imeweka kambi, kuelekea Birmingham Uingereza yalipo makao makuu ya Klabu ya Aston Villa.