KOCHA mpya wa Yanga, Luc Eymael, raia wa Ubelgiji, amefunguka kuwa ametenga wiki moja, sawa na saa 168 kwa ajili ya kukitazama kikosi chake na kusuka kile ambacho anakitaka.
Kocha huyo alitinga Tanzania Alhamisi iliyopita na fasta akapelekwa visiwani Zanzibar ambapo Yanga walikuwa wanacheza mechi ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mbelgiji huyo alitua na kupokelewa na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, ikiwa ni maalum kwa ajili ya kuja kuchukua mikoba ya Mkongomani Mwinyi Zahera ambaye alivunjiwa mkataba.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Eymael amesema siku hizo saba zitatosha kumpa taswira ya wapi aanze napo lakini pia kuunda kikosi chake ambacho atakitumia.
“Nilitazama timu kule Zanzibar lakini hiyo haikutosha, nitawaangalia wachezaji kwa wiki moja kutazama ni nini wanachokifanya.
“Lakini pia kutazama maeneo gani ambayo nahitaji kuyafanyia kazi na kuunda kikosi ambacho nakihitaji.
“Nafanya hayo kwa sababu nipo hapa kufanya makubwa na malengo ni kuwa kati ya timu tatu za juu na baadaye kutwaa ubingwa kwa ajili ya kutinga michuano ya kimataifa, naamini hivyo sababu hakuna ambacho kinashindikana katika soka,” alisema Mbelgiji huyo.
SAID ALLY, Dar es Salaam