Meli ya kubeba mafuta inayopeperusha bendera ya Urusi imegongana na meli ya uvuvi ya Uturuki katika Bahari Nyeusi leo Ijumaa.
Ofisi ya gavana wa mji mkuu wa kibiashara nchini Uturuki, Istanbul, imesema watu watatu waliokuwa katika meli hizo, hadi sasa hawajulikani walipo.
Ajali hiyo inaripotiwa kutokea majira ya saa kumi na mbili asubuhi karibu na Istanbul, na kwamba meli hiyo ya Urusi ijulikanayo kama Glard 2, imeizamisha ya Uturuki, Dursun Ali Coskun.
Gavana wa Istanbul amesema raia watatu wa Uturuki waliokolewa, na shughuli za uokozi bado zinaendelea. Walinzi wa pwani ya Uturuki wamepeleka meli nne na helikopta moja katika katika eneo la ajali.