Meya Dar Atua Kortini, Apinga Kuvuliwa Umeya



MSTAHIKI  Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita,  amewasilisha pingamizi la maombi mawili likiwemo la kuweka zuio la kikao cha kujadili ajenda ya kumuondoa kwenye nafasi yake ya umeya wa jiji la Dar es Salaam.

 

Maombi hayo yamewasilishwa na wakili wa utetezi, Hekima Mwasipu, ambapo ameomba mahakama hiyo itoe zuio la vikao vya halmashauri ya jiji kutojadili ajenda ya kumuondoa meya huyo  kwenye nafasi yake mpaka hapo kesi ya msingi itakaposikilizwa.

 

Mwasipu amesisitiza kuwa ibara ya 13 (6)(a) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  wakati haki ya mtu inaposikilizwa na mahakama au chombo chochote, ana haki ya kusilizwa.

 

Pia katika ombi lingine,  upande huo wa utetezi umeiomba mahakama kesi hiyo iahirishwe kwani imekuja kwa ajili ya kutajwa na si kusikilizwa.

 

Akijibu hoja hizo,  Wakili wa Serikali, Gabriel Malata,  ambaye ni Msaidizi wa Wakili wa Serikali Mkuu amedai kuwa, maombi hayo yameletwa chini ya hati ya dharura na wito waliopelekewa uliwaita kusikiliza kesi na si kwa ajili ya kutajwa, na kwamba upande wa wajibu maombi upo kwa ajili ya kusikiliza shauri hilo.

 

Malata ameeleza mbele ya mahakama kuwa hoja ya zuio la kumuondoa kwenye umeya ni kitu ambacho hakijulikani na mahakama haiwezi kutoa uamuzi kwa mambo ya tuhuma za mitaani na kwamba hakuna mazingira yoyote yaliyokuwa wazi isipokuwa kuna hisia,  na mahakama haiwezi kutoa uamuzi kwa kitu ambacho hakipo kwenye maombi na kusisitiza maombi hayo yaondolewe.

 

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili,  Mtega amesema atatoa uamuzi wa shauri hilo kesho saa nane mchana.

 

 


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad