Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewaagiza maafisa michezo wote chini kubadilika katika utendaji wao kutokana na kulalamikiwa na wadau wengi wa michezo namna ambavyo wanashughulikia sekta hiyo.
Waziri Mwakyembe ametoa agizo hilo Januari 25 Jijini Arusha alipokutana na wadau wa michezo kujadili maendeleo ya sekta hiyo ambapo amewataka maafisa michezo kuhakikisha masuala ya michezo katika maeneo yao hayakwami kutokana na wao kutowajibika.
“Nyinyi ni watumishi wa Serikali mnaposhindwa kutatua kero za wanamichezo na kusimamia sekta hii basi nyie hamtoshi na mimi sitawavumilia kuona mnakwamisha maendeleo ya michezo nchini”, amesema Dkt. Mwakyembe.
Aidha Waziri Mwakyembe ameliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ifikapo Februari mosi 2020 liwe limewasilisha mapendekezo ya mabadilio ya Katiba ya Chama cha Riadha nchini ili kupata muongozo wa mchezo huo.
Serikali pia imerudisha michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA katika shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha sekta hii inaendelea kukua na kuliletea heshima taifa, na kwamba inadhamiria kutofautisha viwanja vya sanaa na vya michezo kwasabu sekta hizi zina wadau wengi ambao wamekuwa na matukio yanayofanana na yanayofanyika kwa wakati unaofanana hivyo ni vyema kila sekta ikajitegema katika maonesho yake.