Molinga Aondoka Yanga Kisa Utovu wa Nidhamu



STRAIKA wa Yanga, raia wa DR Congo, David Molinga, ametimkia nchini na kwenda zake Ufaransa kwa madai ya kwenda kutatua matatizo ya familia yake ambayo inaishi nchini humo.

 

Tangu Molinga atue Yanga msimu huu, ameshafunga mabao manne kwenye Ligi Kuu Bara, pamoja na kudaiwa kutochezeshwa mchezo wao dhidi ya Simba uliopigwa Jumamosi iliyopita kufuatia kile kilichodaiwa kusimamishwa na uongozi huo kwa utovu wa nidhamu aliouonyesha baada ya kufanyiwa mabadiliko kwenye mchezo wao dhidi ya Biashara United.

 

Chanzo chetu kimeliambia Championi Jumatano kuwa, kutokana na adhabu hiyo Molinga aliendelea kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu jambo ambalo limesababisha atupwe nje ya kikosi hicho kiasi cha kuamua kutimkia nchini Ufarasa kuonana na familia yake.



“Molinga hayupo kikosini kwetu tangu tuje hapa Unguja, ila kwa dalili ninazoziona sidhani kama kweli atarejea tena ndani ya kikosi maana amekuwa na tofauti na viongozi tangu siku ile alipofanyiwa mabadiliko katika mchezo wetu na Biashara, ambapo alitoka na kwenda kuvaa nguo zake za nyumbani kisha akataka kulazimisha kukaa benchi wakati kanuni haziruhusu kufanya hivyo.

 

“Nimesikia ameomba ruhusa ili akatatue matatizo ya kifamilia nyumbani kwake Ufaransa maana huko ndipo anakoishi na familia yake na kwamba hakai Congo kama wengi wanavyojua, ninavyoona safari yake hii inaweza kuwa ndiyo ya moja kwa moja na kwamba inawezekana asirudi tena nchini,” kilisema chanzo hicho.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alipoulizwa kuhusiana na hilo hakuwa tayari kusema chochote.

Stori na Musa Mateja



Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad