Mondi Kufuru, Anchokifanya Haijawahi Kutokea




HII sasa sifa! Wakati akiwa na ‘marekodi’ ya kufa mtu, staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameendelea kuziandika mpya ambapo yajayo 2020 yanafurahisha, IJUMAA WIKIENDA lina mchapo kamili.

 

Mkali huyo anayekimbiza na Wimbo wa Baba Lao na ule alioshirikishwa wa Yope ambao ndiyo habari ya mjini kwa sasa, anakuja na kufuru ya mabilioni ya fedha wakati ambao anasherehekea miaka 10 tangu aanze muziki mwaka 2009.

 

Diamond au Mondi, usiku wa kuamkia leo alikuwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma akiangusha bonge la shoo la kuadhimisha miaka hiyo ya kwenye gemu akiwa na wasanii ‘karibu wote’ wa Bongo Fleva, filamu na tasnia nyingine.

 

KUFURU YA 2020 SASA

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, mmoja wa mameneja wa Diamond, Hamisi Shaban Taletale ‘Babu Tale’ amesema mpango wao mpya kwa mwaka ujao 2020 ni kujenga ukumbi mkubwa wa kisasa (arena) endapo watapewa eneo na Serikali.

 

“Kutokana na kwamba kwa sasa Wasafi wana mashabiki wengi, nakumbuka kipindi cha nyuma tulikuwa tunatumia ukumbi tu unatosha, lakini kwa sasa mashabiki wamekuwa wengi tunatumia viwanja ambavyo pia vimeonekana kutokutosheleza kutokana na wingi wa watu hivyo ni wakati sasa wa kujenga arena,” alisema Babu Tale.

 

AZUNGUMZIA YA MBEYA

Babu Tale alisema kilichotokea kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ni dhahiri sasa kinashinikiza wazo lao hilo walichukulie hatua haraka kwani mbali tu na kutofanya uharibifu wa viwanja, bali ni uwekezaji mkubwa.

 

“Kama tulivyoona kile ambacho kimetokea Mbeya kwenye shoo ya Rayvanny, tunatamani kwa kweli kisijirudie tena kwa hiyo endapo Serikali itatupa eneo kubwa, basi Diamond atajenga arena ambayo itaingiza watu wengi na wasipate adha yoyote ile, wala uharibifu wowote ule na eneo likishapatikana ndiyo tutajua tutajenga arena ya aina gani, huwezi kuchagua aina wakati eneo halijapatina bado,” alisema Tale.



MWAKYEMBE AWAITA MEZANI

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta waziri mwenye dhamana ya sanaa, Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na kumfikishia suala hilo la Diamond ambapo alilipokea kwa mikono mwili huku akianisha pia kuwa Serikali inao mpango wa kujenga arena.

 

“Mpango wa kujenga arena kubwa kwa upande wa Serikali upo na tayari kuna kamati ambayo inashughulikia hilo, lakini kama Diamond anataka kushirikiana na sisi tanamkaribisha mezani aje na tutakaa ili tuweze kujadili kwa pamoja tujue namna ya kufanya hiyo arena,’’ alisema Mwakyembe.

 

GHARAMA ZA ARENA

IJUMAA WIKIENDA linafahamu, ujenzi wa arena hizo za kisasa unatofautiana kulingana na mambo mbalimbali ikiwemo uwezo wa kuingiza idadi ya watu, lakini bei zake zinaanzia kwenye Dola za Kimarekani milioni tano (zaidi ya shilingi bilioni 11) hivyo kama Mondi atafanikiwa, basi mradi huo utakuwa miongoni mwa miradi yake mikubwa anayoimiliki.

Nje ya Afrika, zipo arena zinazotajwa kuingiza watu wengi kufikia watu elfu hamsini na kuendelea.

 

ARENA ZA AFRIKA

Miongoni mwa arena kubwa Afrika ni Salle de Sports de Algiers ya nchini Algeria, yenye uwezo wa kuingiza watu 8,000 kwa wakati mmoja, Palais des Sports Kintélé ya nchini Kongo inayoingiza watu 10,000 na The Covered Hall ya nchini Misri inayoingiza watu 20,000.

 

Nyingine ni Ticketpro Dome ya nchini Afrika Kusini inayoingiza watu 20,000, Salle Omnisport de Radès ya nchini Tunisia inayoingiza watu 12,000, Pavilhão Multiusos do Kilamba ya nchini Angola ambayo inaingiza watu 12,000 na Suliman Ad-Dharrath Arena ya nchini Libya ambayo inaingiza watu 10,000.

 

STORI: NEEMA ADRIAN, WIKIENDA


Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. kweli haijawi kutokea, kufanya shoo za bure na kulipia mabehewa 8 kwenda! kigoma Miujiza ya Dunia.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad