MWAMUZI mwenye beji ya Shirikisho la Sola la Kimataifa (Fifa), Omar Abdulkadir, amesema penalti waliyopewa Simba na kuzaa bao la kwanza lililofungwa na Meddie Kagere haikuwa halali.
Lakini mwamuzi mwingine mwenye beji ya Fifa, Othuman Kazi yeye amekuwa na mawazo tofauti akisema ilikuwa ni penalti halali.
Kumekuwa na mjadala mkubwa kama penalti ile ni halali au la baada ya mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2 Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Simba ilipata penalti katika dakika ya 38 kipindi cha kwanza baada ya beki wa Yanga Kelvin Yondani kumvuta mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere kabla ya mwamuzi wa mchezo huo Jonesia Rukyaa kuweka penalti ambayo ilifungwa na Kagere.
Abdulkadir ambaye alistaafu mwaka 2004 akiwa na miaka 45, alisema kuwa kwa upande wake anashindwa kukubaliana kuwa ilikuwa penalti kwa sababu zake tatu alizozitoa huku Kazi yeye akiamini ilikuwa penalti halali.
Abdulkadir alisema kuwa sababu yake ya kwanza ilinayompa ugumu kuamini ilikuwa penalti ni kwa kuwa mwamuzi hakuwepo katika eneo la tukio lakini akaenda mbali zaidi kwa kumtupia lawama mwamuzi msaidizi namba moja, Soud Lila kwa kushindwa kutafsiri tukio hilo.
“Kuna mambo matatu ambayo yananipa ugumu kusema ninachokiona labda ningekuwa nimeangalia tena lakini kwa tukio lilivyotoa mwamuzi alikuwa mbali, sasa sijui kwa nini alisema penalti au alionaje.
“Pili, mwamuzi namba moja yeye ndiyo alipaswa kujua kwamba ilikuwa penalti kwa sababu alikuwa karibu na tukio ila alishindwa kusema kitu na mwisho ukiangalia naona tukio limefanyika nje kabisa ya 18, sasa sijui kipi ambacho kimepelekea hivyo,” alisema Abdulkadir.
Lakini kwa upande wa Othuman Kazi alisema kuwa anaamini penalti ilikuwa sahihi na halali kutolewa na mwamuzi kwa kuwa beki wa Yanga alifanya kosa akiwa tayari ameshakanyaga mstari wa eneo la 18.
“Kisheria naona mwamuzi alikuwa sahihi kutoa ile penalti kwa sababu tukio limetokea wakati wameshakanyaga mstari wa eneo la 18, hivyo alichokiamua kilikuwa sahihi kabisa,” alisema Kazi wakati alipokuwa akichambua tukio hilo kwenye kituo cha Azam TV.
Championi lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Chama ambaye alisema kuwa kwa upande wake anawapongeza waamuzi wake kwa kuwa walichezesha bila ya upendeleo wowote licha ya kuwa na upungufu wa kibinadamu.
“Binafsi naona waamuzi wangu wamechezesha vizuri lakini nawapa alama 95 katika mchezo ule na alama tano ni za makosa ya kibinadamu ambaye mtu yeyote anaweza akafanya.
“Unajua huwezi kufanya kila kitu kikawa sawa ndiyo maana wenzetu Ulaya wanatumia teknolojia ya VAR kwa ajili ya kusaidia kutoa maamuzi kwenye matukio tata lakini kwa Afrika bado kutokana na changamoto ya kiuchumi katika mashirikisho yetu,” alisema Chama.