WAKATI mashabiki wa soka hapa nchini wakiendelea kupishana kauli juu ya mshambuliaji wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere kuwa alikuwa na hirizi uwanjani katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga huku wengine wakipinga, Championi Jumatano limepata ukweli wa jambo hilo.
Simba na Yanga zilicheza Jumamosi iliyopita kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Taifa.
Katika mitaa mbalimbali hapa nchini jambo hilo limekuwa gumzo kubwa lakini kila mtu amekuwa akisema la kwake bila ya kuwa na ukweli wowote.
Hata hivyo, kutokana na hali hiyo mmoja wa waamuzi waliochezesha mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa, ameliambia gazeti hili kuwa, Kagere hakuwa na hirizi katika mchezo huo kama wengi wanavyofikiria.
“Watu wengi tumetawaliwa sana na mawazo ya ajabu na yasiyokuwa na faida yoyote katika maendeleo ya soka letu.
“Kagere hakuwa na hirizi katika mchezo huo bali ile ilikuwa ni cheni ambayo aliokota uwanjani na kumpatia mwamuzi Jonesia Rukyaa ambaye pia aliipeleka kwa mwamuzi wa akiba naye akaipeleka katika benchi la ufundi la Simba.
“Kwa hiyo, hao wanaosema kuwa Kagere alikuwa na hirizi katika mchezo huo ni waongo, niwaombe tu wasiwe wepesi wa kusema vitu wasivyokuwa na uhakika navyo, hata kama utamuuliza Rukyaa naye atakwambia hivyo hivyo, japokuwa maadili hayaturuhusu kusema chochote kabla ripoti zetu kufanyiwa kazi na TFF,” alisema mwamuzi huyo kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini.
Stori: Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam