THERESIA MUMBI ni mama wa mtoto wa kiume mwenye miaka saba, yeye ana miaka 34 , kazi yake ni utingo wa magari ya uchukuzi katika mji mkuu wa Nairobi nchini Kenya.
Lakini maisha yake huwezi kusema ni ya kawaida kama ya mwanamke mwingine, kutokana na kuwa na ndevu nyingi kama mwanaume.
Ilikuwaje akawa na ndevu?
“Nilipokuwa shuleni nilikuwa na nywele nyingi, kwangu mimi niliona kwamba ni jambo la kawaida, hivyo hazikunisumua sana,” Mumbi alisema.
Alipomaliza shule ya sekondari na kuanza kutafuta ajira, mwaka 2005 aligundua kwamba nywele zake zilikuwa zinakua kwa kasi mno, hivyo aliamua kuanza kuzinyoa, lakini kumbe aliharibu na kuzifanya ndevu hizo kukua zaidi.
Theresia anasema kuwa aliogopa sana maisha yake yatakuwaje?
“Niliona kuwa ni kazi ngumu ya kuficha hali hii ya kunyoa ndevu kila wakati, kwani nilikuwa nazinyoa kila saa, na nikaanza kuchoka nikaamua kuwa sitazinyoa tena” alisimulia Mumbi.
Wakati alipokuwa na desturi ya kunyoa hakuwa na changamoto zozote kwani alifanana kama wanawake wengine wa kawaida.
Pale alipoacha kunyoa, masaibu mapya yalianza, kwani alikuwa ana mwonekano mwingine, alianza kuandamwa na watu kwa kumwangalia kwa kumshangaa na kumnyooshea kidole, huku wakimpa majina ya kejeli.
Wakati huo alikuwa anafanya kazi kama mhudumu katika hoteli moja mjini, ilikuwa rahisi kwake kwani wale wateja wake walikuwa wamezoea mwonekano wake wa ndevu, ila matatizo yalikuwa wakati alipokuwa nje ya eneo lake la kazi.
“Nikiwa nyumbani nilikuwa sitoki nje kabisa, hata kama ningekuwa na njaa vipi, nilikuwa nasubiri hadi giza liingie ilimradi niende dukani au sokoni kununua mboga au chakula,” Mumbi aliongezea kusema
“Nilikuwa naona aibu ili jirani zangu wasinione na ndevu halafu waanze kuzua gumzo mtaani, ingawa sikuwa na shida na sehemu yangu ya ajira,” alieleza.
Haya yote yalichangiwa na kuwa ndevu zake zilikuwa zinakua na pia alikuwa amechoka kunyoa kila wakati, pamoja na kuwa ngozi yake iliharibika na aliogopa kujichibua zaidi.
Mumbi aliamua kutafuta msaada wa daktari ambapo aliambiwa kuwa mwili wake ulikuwa na hitilafu ya homoni, na hilo lilimsababishia yeye kuwa na nywele hizo.
Kisa kimoja ambacho Mumbi hatawahi kukisahau ni wakati alipokamatwa na maofisa wa polisi akiwa kazini.
Siku hiyo anasema kuwa ilikuwa tofauti kwani anadai kuwa maofisa waliwataka kila mtu atoe shilingi mia nne za Kenya au apelekwe rumande, Mumbi anasema kuwa hakuwa na hela hizo.
Kwa hiyo yeye na baadhi ya wahudumu wa magari ya matatu (daladala) walipelekwa katika kituo cha polisi, walipofika huko yeye aliwekwa katika sehemu ya wanawake, baada ya muda ofisa mmoja wa kike aliingia kwenye gereza alimokuwa Mumbi na kumuamrisha atoe nguo zake, alipomuuliza kwa nini? alimjibu:
“Hatuna uhakika kuhusu jinsia yako na tunahofia kuwa wewe ni mwanaume, kwa hivyo tunataka kukukagua ili tuthibitishe,” Mumbi alisema
Mumbi anasema tukio hilo lilimhuzunisha sana kwani polisi hao walimdhalilisha kwa kuwa alikuwa na ndevu.
Mumbi anasema kuwa kitendo kile kilimfanya alijiulize maswali mengi na pia kumuuliza Mwenyezi Mungu maswali ya kwa nini alimuumba akiwa hivyo ?
Alijiuliza na kuhisi ikiwa polisi walimfanyia hayo, je raia nao wangemfanyia nini kutokana na hali yake? Anasema kuwa hakuweza kupigania haki yake licha ya kudhalilishwa na polisi.
Haikuwa rahisi kwani wakati mmoja alihisi kujitoa uhai wake, lakini mojawapo wa sababu za kwa nini hajaweza kuafikia hayo na kuziondoa fikra hizo, ni kutokana na mwanaye, ambaye yeye amemkubali jinsi alivyo na amempa nguvu ya kuishi maisha yake kama wengine.
Je ni kawaida kwa wanawake kuwa na ndevu ?
Kwa mujibu wa wataalam wa afya ya uzazi, wanawake ambao hupata ndevu wanatambulika kwa lugha ya kisayansi kama ‘hirsutism’ au ‘hypertrichosis’.
Vilevile watalamu wanasema kuwa wanawake wengine huenda wakawa na ongezeko la homoni ambayo inapatikana kwa wanaume inayojulikana kama ‘Androgen’ kupita kiasi, hadi sasa hakuna tiba ya kuzuia wanawake kupata ndevu.
Je, kuna wanawake wengine duniani wenye changamoto hizi?
Mmojawapo wa watu maarufu duniani ambao waliibuka na kuzungumzia hali yao ya kuwa na ndevu ni mwanamke kwa jina Harnaam Kaur kutoka Uingereza, mwenye asili ya bara la Asia.
Yeye ni mwanamitindo na pia ni mwanaharakati ambaye anatetea wanawake wenye maumbile tofauti. Alitajwa kwenye kitabu cha kumbukumbu za historia cha ‘Guiness World Records’ kama miongoni mwa wanawake watano ambao ni mashuhuri katika kazi zao.
Kabla hajajikubali, Bi Kaur alikuwa amejaribu kuondoa ndevu zake bila mafanikio, kwa kuwa alikuwa anakabiliana na kejeli na hujuma nyingi kutoka kwa umma, ila sasa ametambulika kama mtetezi wa wanawake ambao wana ndevu duniani.
Katika nchi za Bara la Afrika baadhi ya wanawake kutoka nchi za Malawi, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Nigeria inasadikiwa kwamba kuwa na ndevu ni ishara ya kuwa na kizazi chema. Lakini katika mataifa mengine wanawake kama hao hunyanyapaliwa.