Chama tawala cha Burundi CNDD-FDD, kimemteua katibu wake mkuu kuwa mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa Burundi utakaofanyika Mei 2020.
Jenerali Evariste Ndayishimiye ameidhinishwa na chama kama mrithi wa Nkurunziza wa Burundi.
Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye ameteuliwa kama mgomba wa urais katika uchaguzi utakaofanyika Mei 2020 kumrithi Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Jenerali Ndayishimiye ameteuliwa Jumapili kupeperusha bendera ya chama cha CNDD-FDD katika kikao kisicho cha kawaida kilichofanyika Gitega, mji mkuu wa kisiasa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa saa tatu ya chama tawala cha CNDD-FDD.
Bwana Ndayishimiye ni miongoni mwa wanasiasa mashuhuri katika siasa za Burundi waliokaribu na Pierre Nkurunziza.
Pia ni miongoni mwa waliokuwa waasi wa CNDD-FDD aliyejiunga baada ya kunusurika katika mauaji ya kikabila ya wanafunzi wa Wahutu katika chuo kikuu cha Burundi mwaka 1995.
Jenerali Ndayishimiye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa chama cha CNDD-FDD tangu Agosti 2016.
Kabla ya kuteuliwa kwake, alikuwa Waziri wa mambo ya ndani na ulinzi wa umma.
Baada ya chama cha CNDD-FDD kusaini makubaliano ya Amani ya 200 kuratibu kikosi cha taifa cha jeshi la ulinzi, Ndayishimiye alichaguliwa kama msimamizi mkuu wa jeshi na kuwa msaidizi wa jeshi wa Rais Nkurunziza.
Mwak 2018, Rais Pierre Nkurunziza alitangaza kwamba hatasimama tena katika kinyang'anyiro cha kugombea urais baada ya kubadilisha katiba ya nchi, hatua ambayo ilionekana na wengi kama njia ya wazi ya kutaka kusalia madarakani milele.
Awali wiki iliyopita, Bunge la Burundi lilipitisha sheria ya marupurupu ya kustaafu ya $530,00, jumba la kifahari na mshahara mzuri tu wa kila mwezi kwa kipindi kilichosalia hadi Bwana Nkurunziza atakapoondoka madarakani.
Uamuzi wake wa kugombea tena urais kwa awamu ya tatu mwaka 2015 ulisababisha nchi hiyo kuingia katika machafuko.
Kuchaguliwa kwa Meja Jenerali Ndayishimiye huenda kukawa mwanzo mwema wa kuondoa machafuko ya kisiasa yaiyoshuhudiwa mwaka 2015 na kutengeneza mazingira thabiti kwa Burundi.