Polisi Matatani Kwa JARIBIO la Kubambika Kesi ya Utakatishaji
0
January 06, 2020
Moshi. Watu watano wakiwamo wanaodaiwa kuwa askari polisi wawili wa kituo cha Himo mkoani Kilimanjaro wanatuhumiwa kumteka mfanyabiashara wa mjini Moshi na kumbambikia tuhuma kisha baadaye kumwomba rushwa ya Sh140 milioni.
Baada ya kumkamata, watu hao ambao awali inadaiwa walijitambulisha kama maofisa wa idara ya usalama wa Taifa, walizunguka na mfanyabiashara huyo kwa mawakala wa Benki ya CRDB ili atoe fedha hizo.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, James Manyama alipoulizwa juzi alikiri kuwapo kwa malalamiko hayo lakini akasema suala la polisi wanaotajwa kuhusika, litashughulikiwa kiutawala.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa askari hao walikubali wapewe Sh30 milioni baada ya kujadiliana kwa saa kadhaa kutokana na awali kutaka Sh140 milioni baada ya kumtisha mfanyabiashara huyo kuwa anakwenda kushitakiwa kwa kosa la utakatishaji fedha.
Awali gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Salum Hamduni ambaye alisema hajapewa taarifa hizo na kuahidi kufuatilia baada ya mwandishi wetu kumpa namba ya jalada.
Suala hilo limefunguliwa jalada namba MOS/RB/79/2020 katika kituo kikuu cha Polisi mjini Moshi ambapo polisi wawili wa kituo cha Himo walitambuliwa na mlalamikaji wakiwa ni miongoni mwa watu watano wanaodaiwa kumteka.
Taarifa hizo zinadai Januari 2, 2020 huko geti la kuingia Mlima Kilimanjaro, watu hao inadaiwa walikula njama na kumtuma mmoja wa washirika wao, kwenda kwa mfanyabiashara huyo kwa ajili ya kubadili Dola 100 za Marekani.
Akizungumza jana, mfanyabiashara huyo, Julius Mlay, alidai siku ya tukio alifika mtu aliyewahi kuwa askari wa Kinapa (Mbuga ya Kilimanjaro) kabla ya kufukuzwa kazi, akaomba ambadilishie Dola 100 za Marekani.
“Huyo bwana namfahamu kwa hiyo akaniambia ana wageni wake wanataka kwenda `day trip’ (matembezi ya siku moja) na hawana hela ya Tanzania ambayo anatakiwa kuweka kwenye simu,” alidai.
“Utaratibu ni kuwa huwezi kulipa `cash’ (fedha taslimu) getini kwa hiyo akaomba nimpe Sh220,000 aniachie ile Dola 100 na baada ya wageni wake kupanda na kushuka angechukua dola zake,” alisimulia mfanyabiashara huyo.
Mfanyabiashara huyo anadai ghafla wakati amempa fedha hizo kwa ahadi atazirudisha na kuchukua dola yake, walitokea watu hao watano waliojitambulisha ni maofisa usalama wa Taifa.
“Walinikamata na kuniambia watu kama mimi ndio Rais Magufuli anawatafuta washitakiwe kwa utakatishaji fedha. Wakasema nitakaa gerezani miaka mitano ndio nihukumiwe,” alidai.
Lakini alidai kabla ya kuondoka eneo hilo, walifanya upekuzi katika ofisi yake na kukuta Sh2 milioni kwenye droo ambazo walizichukua na kumweleza anatakiwa kusafirishwa kwenda Dar.
“Tukiwa njiani tunaelekea Himo na mimi niko katikati yao wakaniambia nijiongeze kwa kuwa nina tuhuma nzito. Nikawaomba wanisameheme wachukue ile Sh2 milioni waliyochukua,” alidai.
Hata hivyo, mfanyabiashara huyo alidai mmoja wao aliyedai kuwa ndio bosi alidai kuwa alimtishia kuwa anawachezea na akamwambia bila Sh140 milioni, watampoteza njiani wakati wakielekea Dar es Salaam. “Niliwaomba sana ndio mwisho wakaishia Sh30 milioni. Wakaniambia twende kwa wakala wa CRDB hawataki kwenda benki kwa sababu huko kuna kamera za CCTV,” alidai Mlay.
Kwa mujibu wa Mlay, alisema walimpeleka kwa wakala aliyepo kituo cha mafuta cha Panone Chekereni akawa hana pesa, wakapiga simu Himo akatokea wakala akasema ana pesa.
“Tulivyofika kwa huyo wakala akasema kiwango cha mwisho kutoa ni Sh5 milioni. Akaniambia ingiza namba ya siri. Nikaikosea makusudi mara tatu kadi ikajifunga,” aliongeza.
“Huyo bosi wao akasema huyu tukamweke mahabusu hadi kesho yake lakini mmoja akasema huyu anaonyesha ni mwaminifu tumwachie ili kesho yake nitoe fedha benki niwapelekee,” alidai.
Alidai siku iliyofuata walianza kumpigia simu saa 2:00 asubuhi kumuulizia kama ameshaenda benki na usumbufu huo uliendelea, na alipoomba ushauri kwa marafiki walimwambia atoe taarifa polisi.
“Nikaenda kituo cha polisi cha Himo lakini nilipokuwa nataka kuanza kuandika maelezo nikamuona mmoja ananiangalia sana. Polisi mmoja akanishauri niondoke kwa siri nikafungue jalada Moshi mjini,” aliongeza.
Hata hivyo taarifa zinadai mmoja wa maofisa wa polisi ngazi ya wilaya, alipendekeza suala hilo limalizwe kidiplomasia ambapo maofisa hao wa polisi walikubali kurejesha Sh2 milioni.
Taarifa hizo zinadai tayari maofisa hao wa polisi wameomba kurejesha Sh2 milioni pamoja na Dola 100 walizochukua na juzi Januari 4, 2020 walirejesha Sh500,000 na kuahidi watamalizia Januari 30, 2020.
Tukio hilo limekuwa gumzo miongoni mwa wafanyabiashara wanaohudumia watalii, wakitaka suala hilo lichukuliwe kama unyang’anyi wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka ya polisi hao.
Mwananchi
Tags