Polisi nchini Iran katika mji mkuu Tehran, wamekanusha kutumia silaha dhidi ya waandamanaji walioghadhabishwa na kudunguliwa kwa ndege ya Ukraine.
Mkuu wa Polisi mjini Tehran Hassan Roheimi ametoa taarifa hiyo baada ya vidio zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha polisi wakiwafyatulia risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi waandamanaji.
Video hizo zilizowekwa kwenye mitandao na shirika la kutetea haki za binadamu lililo na makao yake New York lakini hazikuweza kuthibitishwa kwa wakati huo.
Maandamano yalianza Jumatatu baada ya Iran kukubali kwamba ilirusha kombora kimakosa dhidi ya ndege ya abiria ya Ukraine na kuanguka karibu na Tehran.
Watu wote 179 waliokuwa kwenye ndege hiyo PS752, wengi wao wakiwa raia wa Iran na Canada walikufa.