Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amewazuia Mabalozi wanaowakilisha nchi katika Mataifa mengine, kuendelea na tabia ya kizamani ya kwenda kuaga kwa kila kiongozi wa Serikali.
Rais Magufuli ameyabainisha hayo leo Januari 14, 2020, mara baada ya zoezi la kuwaapisha Mabalozi wa nchi nne ikiwemo Zimbabwe, Nigeria, Afrika Kusini pamoja na Namibia, hafla iliyofanyika Ikulu ya Jijini Dar es Salaam, na kumuagiza Waziri wa Mambo ya Nje kuhakikisha barua za Mabalozi hao zinapatikana haraka ili waweze kwenda kufanya majukumu yao waliyopangiwa.
“Ninajua siku za nyuma kulikuwa na tabia ya watu, akishateuliwa Ubalozi atakaa tena anazunguka maofisi kwenda kuaga kwa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Nje wengine wanaenda hadi kwa Wakurugenzi na Wakuu wa Mikoa, ikiwezekana ndani ya wiki 2 muwe mmeshaenda kwenye hizo nchi ambazo mtatuwakilisha” amesema Rais Magufuli.
Walioapishwa leo ni Meja Jenerali Mstaafu, Gaudence Milanzi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Dkt Modestus Francis Kipilimba kuwa Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Profesa Emmanuel David Mwaluko Mbennah, kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe pamoja na Dkt Benson Alfred Bana kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria.
By Ally Juma.