Rugemalira Ameileza Mahakama Kuwa Upelelezi wa Kesi inayowakabili Hautakaa Ukamilike


Mfanyabiashara James Rugemalira ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi dhidi ya kesi yao ya uhujumu uchumi inayomkabili yeye na wenzake hautakaa ukamilike mpaka pale watakapofuatilia barua waliyomuandikia  Kamshina Generali wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Rugemarila amedai hayo leo Januari 30,2020 mbele  ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi wakati kesi yao hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru Maghela Ndimbo kuieleza mahakama kuwa upelelezi dhidi ya kesi hiyo bado haujakamilika.

 Mshtakiwa Rugemalira baada ya kusikia hayo alinyoosha mkono na alipopewa nafasi ya kuzingumza alidai,  amemuandikia barua Kamishna Generali wa TRA akimuelezea ni jinsi gani benki ya Standard Charter Hong Kong walivyokuwa wakikwepa kodi na ushuru wa forodha.

Rugemalira alidai kuwa Januari 24, mwaka huu, aliongea na mwakilishi wa Takukuru alipomtembelea gerezani na akamkabidhi nakala ya barua hiyo aliyoandika kwenda kwa Kamishna  wa TRA lakini hadi sasa hajapata jibu lolote.

"Naomba kesi ikija kutajwa tena upande wa mashtaka walete jibu kwa  sababu wanaostahili kushitakiwa katika kesi hii ni benki hiyo na ninashangaa kuona wengine wanaongezwa  katika kesi kwa madai upelelezi haujakamilika," amedia Rugemalira na kuongeza kwamba upelelezi wa kesi hiyo hautakamilika na  ili  ukamilike wafuatilie hiyo barua aliyowapelekea.

Mbali na Rugemalira,  washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme, (IPTL)  Harbinder Sethi na aliyekuwa mwanasheria wa kampuni hiyo, Joseph Makandege.

Kutokana na  maelezo hayo ya Rugemalira Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo mpaka  Februari 13, 2020 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Washtakiwa Sethi na Rugemalira walifikishwa mahakamani hapo  zaidi ya miaka miwili wamekaa rumande, kutokana na upelelezi wa kesi yao kutokukamilika.

Washitakiwa Seth na Rugemalira kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27 kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, mwaka 2017.

Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Aidha, inadaiwa katika mashitaka ya kujipatia fedha kwamba  kati ya  Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika Makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni  na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph,  kwa ulaghai washitakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dola za Marekani  22,198,544.60 na Sh 309, 461,300,158.27.

Pia washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la  kati kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dola za Marekani milioni 22.1 na Sh bilioni 309.4  wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Mshtakiwa Makandege  anakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuisababishia  serikali hasara ya dola za Marekani 980,000 pia yapo ya utakatishaji wa Fedha.

Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka hayo Desemba 20,2019,baada ya kuunganishwa na washtakiwa Seth na Rugemalira katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi.

Miongoni mwa mashtaka hayo ,Makandege anadaiwa kuwa, kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Kenya, Afrika Kusini na India, akiwa na wenzake walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Pia anadaiwa  kuongoza genge la uhalifu,  katika nchi hizo, akiwa si mtumishi wa Serikali akishirikiana na watumishi wa umma kwa kuratibu na kufadhili mpango wa uhalifu.

Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Makandege anadaiwa kuwa kati ya Januari 23, 2014 na Februari 2014, alijipatia dola 380,000 katika benki ya Stanbic iliyopo Kinondoni na dola 600,000 katika benki ya UBL Bank(T) Ltd iliyopo wilaya ya Ilala, fedha zilizotoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa nyakati tofauti.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad