MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi, Januari 16, 2020, imemuamuru Mfanyabiashara, James Rugemarila kufika mahakamani akiwa na vithibitisho vya Hospitali katika tarehe tajwa.
Hiyo imekuja baada ya hakimu Mkazi Mwandamizi, Vicky Mwaikambo kutaka kujua sababu ya kutofika mshtakiwa huyo mahakamani ndipo mmoja wa askari magereza alidai kuwa Rugemarila ni mgonjwa hivyo ameshindwa kufika.
Mwaikambo amesema amepokea taarifa ya kuumwa kwa Rugemarila hivyo shauri litakapokuja tarehe ijayo mshtakiwa huyo hakikishe anapeleka vithibitisho vya hospitali.
Wakili wa Takukuru, Godliver Kiriani amedai kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Kesi hiyo limeahirishwa hadi Januari 30, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa. Mbali na Rugemarila wengine mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Seth, na Mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege ambaye aliunganishwa katika kesi hiyo Desemba 20 mwaka jana.
Miongoni mwa Mashtaka yanayowakabili ni pamoja na kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kuisababishia Serikali hasara na kutakatisha fedha.