Sakata la Kumng’oa Meya wa Dar Lazua tafrani, Anyang’anywa Gari




MEYA Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amejikuta njia panda baada ya kunyang’anywa gari alilokuwa akilitumia ambalo linamilikiwa na halmashauri hiyo muda mchache baada ya uamuzi wa mkutano mkuu kutoa uamuzi dhidi ya tuhuma dhidi yake.

 

Mkutano huo umefanyika leo Alhamisi, Januari 9,2019 katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee wilayani Ilala, Dar es Salaam chini ya ulinzi wa Polisi.

 

Akisoma matokeo ya azimio la wajumbe waliopiga kura ya kutokuwa na imani na Mwita, Naibu meya Abdallah Mtinika aliyekuwa akiongoza kikao hicho idadi ya waliopigwa kura kwa kusimama kwenye viti vyao ni 16.

 

“Naomba nisome uamuzi wa mwanasheria wetu wa jiji la Dar es Salaam, kuhusu uamuzi wa kutokuwa na imani ya meya.”

 

“Kura zilizopigwa ni 16 na mjumbe mmoja ameomba udhuru na wawili hawakupiga kura, uamuzi wenu umepitishwa, baada ya hapo nafunga kikao,” amesema Mtinika.

 

Hata hivyo, Mtinika hakusema kama Mwita ameondolewa katika nafasi badala yake alisema uamuzi wa wajumbe 16 ambao ni CCM. Hata hivyo baada ya kutoa uamuzi huo wajumbe wa Chadema walionekana wakishangilia na kusema kuwa bado Mwita ni meya wa jiji hilo.”

 

Meya wa Ubungo, Boniface Jacob amesema kwa mujibu kanuni  ili Mwita aondolewa ilitakiwa ipatikane theluthi mbili ambao ni wajumbe 17, lakini CCM walikuwa 16.

 

Baada ya kutoka nje ya ukumbi Mwita alikwenda moja kwa moja  katika maegesho ya magari ambako hakulikuta gari aina Prado alilokuwa  akilitumia katika shughuli zake za kila za nafasi hiyo.

 

Hata hivyo, Mwita amesisitiza yeye bado meya wa jiji hilo kwa kuwa kikao hicho hakijatimiza akidi ya kumuondoa katika wadhifa huo kwa mujibu wa kanuni.

 

“Nashangaa nimenyang’ nywa gari na bendera imeshushwa nawaambia mimi bado ni meya. Namuomba Rais John Magufuli aingilie kati suala hili kwa sababu wakati naingia madarakani ilikuwa hivi hivi.”

 

“Sio gari tu hadi ofisi imefungwa sielewi kinachoendelea dhidi ya wadhifa wangu. Nasisitiza mimi bado meya wa jiji hili,” amesema Mwita.

 

Kikao hicho kilikuwa na lengo la kupokea taarifa ya uchunguzi dhidi ya tuhuma za Mwita baada ya tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  kuchunguza tuhuma ambazo zinamkabili.

 

Miongoni mwa tuhuma anazokabiliana nazo Mwita ni kutotumia Sh 5.8 bilioni za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda). Fedha hizo ni asilimia 51 ya hisa zilizotolewa na kampuni ya Simon Group kama sehemu ya ununuzi wa asilimia 51 ya hisa za Uda.

 

Tuhuma nyingine ni kutumia vibaya gari ya ofisi ambayo alipata nalo ajali, kushindwa kuongoza kikao cha baraza la madiwani na kusababisha meya wa Ubun-go Boniface Jacob kugombana na meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo na kudaiwa kuwapendelea baadhi ya mameya kuingia kwenye kamati za fedha.

 

Hata hivyo, Mwita ambaye pia mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, alishajibu tuhuma hizo akisisitiza hahusiki na jambo hilo bali ni za kutengenezwa ili kuondolewa katika kiti hicho alichokitumikia kwa miaka minne.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad