KAMPUNI ya Samsung kushirikiana na Advanced Research Lab (Star Lab) wamefanikiwa kutengeneza watu wasio asilia ambao watakuwa wanafanana na binadamu katika maeneo mbalimbali ya miili yao kama sura na muonekano, kuonyesha hisia, tabia na akili na pia wana uwezo wa kuzungumza na kubadilishana maongezi kama binadamu wa kawaida.
Watu hao si roboti kwa sababu roboti huwa anamilikiwa kila kitu na binadamu (kwamba bila kupata msaada wa binadamu hawezi kufanya kazi).
Lakini watu hao waliopewa majina ya NEON wataweza kujisimamia wenyewe kwa kila kitu, pia wanaweza kufanya kazi mbalimbali kama vile kusoma taarifa ya habari, anaweza kuwa mwalimu, mshauri wa masuala ya fedha, na hata msimamizi wa mazoezi (gym master). Pia, wanaweza kuwa msemaji wa mtu au kampuni lakini pia wanaweza kuwa waigizaji.
Mtaalamu kutoka Star Lab amesema hawana lengo la kuondoa ajira za binadamu wa kawaida (sisi) ila lengo lao ni kuboresha zaidi maingiliano ya kibiashara baina ya mtoa huduma na mteja.
Watu hao waliotambulishwa Jumatatu ya wiki hii watapatikana dunia nzima kwa ajili ya huduma mbalimbali. Samsung ndiyo wamekuwa kampuni ya kwanza kutengeneza watu wasio asilia (Artificial Human).