Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema uchumi wa taifa umekuwa kwa asilimia 7.0 katika mwaka 2018 na kufanya iwe nchi ya kwanza kwa ukuaji wa uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na nchi ya pili kwa nchi za Afrika Mashariki.
Kauli hiyo imetolea leo Jumanne Desemba 31, 2019 na Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania, Dk Philip Mpango wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2019 na tathimini ya awali ya utekelezaji wa bajeti kwa nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/20.
Waziri Mpango amesema katika kipindi cha Januari - Juni 2019, pato la taifa lilikuwa kwa asilimia 6.9 ikilinganishwa na asilimia 6.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.
Amesema Tanzania ilikua nchi ya tano katika ukuaji wa uchumi Sadc ikitanguliwa na Eritria ambayo uchumi wake ulikuwa kwa asilimia 12.2, Rwanda (8.6), Ethiopia (7.7) na nchi ya Ivory Coast iliyofikisha asilimia 7.4.
Amesema ukuaji huo ulichochewa na kuongezeka kwa uwekezaji hasa katika miundombinu ya barabara, reli, na viwanja vya ndege, kutegemea kwa upatikanaji wa nishati ya umeme, kuimarika kwa huduma za usafiri na usafirishaji pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa madini.
“Kingine ni kuongezeka kwa mazao ya kilimo kutokana na hali nzuri ya hewa lakini sekta zilizokuwa kwa kasi katika kipindi cha kwanza cha 2019 ni ujenzi ambayo imefikia asilimia 16.5, uchimbaji wa madini yenye asilimia 13.7, habari na mawasiliano 10.7, maji asilimia 9.1 pamoja na sekta ya usafirishaji na uhifadhi mizigo iliyofikisha asilimia 9.0,” amesema Mpango.
Kwa mujibu wa Waziri, ukuaji wa uchumi katika mwaka husika unaonekana kupitia upatikanaji wa huduma bora zaidi kwa wananchi zilizotolewa na serikali yao ikilinganishwa na ilivyokuwa katika mwaka uliotangulia.