Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Faustine Bee, amesema mwanafunzi Masumbuko Mgaya alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa makosa 3 ya matumizi ya mtandao na hakuna kosa linalohusiana na suala la upatikanaji wa maji chuoni hapo.
Profesa Bee, ametoa ufafanuzi huo kwa kusema, baada ya kijana huyo kushikiliwa na baadaye alifanikiwa kupewa dhamana, baada ya kukamatwa Januari 22 na 23, 2020.
Mwanafunzi huyo anayesoma Shahada ya Sayansi katika Fizikia (Bachelor of Sciencein Physics), mwaka wa tatu, alishikiliwa na Jeshi la Polisi hivi karibuni huku habari mbalimbali zikielezwa, alikamatwa kwa sababu ya kusambaza picha za uhaba wa maji chuoni hapo.
"Masumbuko Mgaya Juma, anatuhumiwa kwa kutenda makosa matatu tofauti ya kimtandao, ambayo hayana uhusiano na tatizo la ukosefu wa maji, ambalo hata hivyo lilikwishatatuliwa na kutolewa ufafanuzi na Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo, katika taarifa iliyotolewa kwa Umma Januari 20, 2020", imeeleza taarifa hiyo.