Ujerumani itaondoa baadhi ya wanajeshi wake waliowekwa kama sehemu ya muungano unaopambana dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, nchini Iraq, wizara ya ulinzi imesema leo, katika hatua ya kutoridhishwa na shambulio la Marekani la ndege isiyokuwa na rubani ambalo limemuuwa jenerali wa ngazi ya juu wa Iran.
Kiasi cha wanajeshi 30 waliowekwa mjini Baghdad na Taji wataondolewa na kupelekwa nchini Jordan na Kuwait, msemaji wa wizara ya ulinzi ameliambia shirika la habari la AFP, na kuongeza kwamba kuondolewa huko kutaanza hivi karibuni.
Shirika la habari la Ujerumani, dpa, limesema Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer na Waziri wa Mambo ya Kigeni Heiko Maas wamewaandikia wabunge kuwa wanajeshi walioko katika vituo mjini Baghdad na Taji nchini Iraq wataondolewa kwa muda.
Mawaziri hao wawili wamesisitiza kuwa mazungumzo na serikali ya Iraq kuhusu kuendelea na kikosi cha kutoa mafunzo kwa vikosi vya Iraq yataendelea.