MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeagizwa kuongeza muda wa kufanya kazi ya uandikishaji na uchakataji wa taarifa kwa ajili ya vitambulisho vya Uraia kutoka saa nane hadi 16.
Agizo hilo ni kuhakikisha wananchi wanapata vitambulisho au namba kwa ajili ya kukamilisha zoezi la usajili wa laini za simu zinazotarajiwa kufungwa baada Januari 20 mwaka huu.
Pia wameagizwa kuhakikisha wanaongeza wafanyakazi (watendaji wa dharura) katika vituo vya kuandikishia ambavyo vipo katika kila wilaya nchini.
Maagizo hayo yalitolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni jana alipotembelea ofisi za NIDA Kibaha mkoani Pwani ili kujionea zoezi hilo linavyoendelea.
Masauni mbali na kuwaagiza NIDA kufanya kazi kwa saa 16 pia amefuta likizo na mapumziko ya mwisho wa juma kwa wafanyakazi wote wanaofanya kazi katika kitengo cha uchakataji wa taarifa za vitambulisho vya uraia ili kuwezesha wananchi wote kupata vitambulisho kwa wakati.
Masauni alisema wameamua kuongeza muda wa ziada wa kufanya kazi kwa wafanyakazi hao baada ya kutembelea kitengo hicho na kubaini kuwa kuna changamoto ya wafanyakazi wachache na wanafanya kazi kwa saa chache huku wananchi wakiendelea kuhangaika kupata vitambulisho kwa ajili ya kusajili laini zao.
“Lakini vitu ambavyo nimeviona vya msingi na tumekubaliana vifanyiwe kazi haraka, ni kitengo kinachohusika na uchakataji ama uchunguzi wa taarifa mbalimbali ambao kasi yao ni ndogo sana.
“Na kasi hii ndogo inatokana na kwanza uchache wa wafanyakazi na pia uchache wa muda wa kufanya kazi, kwa maelekezo yangu na ambavyo tumekubaliana kwanza wataongeza muda wa kufanya kazi kutoka saa nane hadi 16 kwa siku zote 18 na hakutakuwa na ‘holiday’ likizo wala hakutakuwa na weekend (mapumziko ya siku za mwisho wa wiki)”alisema Masauni.
Alisema pia ameagiza NIDA kuongeza wafanyakazi wa dharura ili kuongeza nguvu.
“Vile vile tumekubaliana kwamba tutawatumia
wafanyakazi wa dharura kwa ajili ya kuongeza nguvu katika makao makuu ya NIDA kwa lengo la kuweza kuchakata zile taarifa za kiuchunguzi”aliongeza Naibu Waziri huyo wa Mambo ya Ndani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa NIDA, Dk. Arnold Kihaule alimuhakikishia Naibu Waziri kuwa ofisi zake kila wilaya zinafanya kila liwezekanalo kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati na kuahidi kuwa watafanya kazi saa 24 siku zote za juma.
“Sisi NIDA kwa upande wetu tunamhakikishia Waziri kuwa tunafanya kazi saa 24, tunafanya kazi jumamosi na jumapili na kwa ushahidi tumefungua kituo Mnazi mmoja tangu Disemba 22 mwaka jana hivyo hatukuwa na Krisimas, Boxing day wala Mwaka Mpya,”alisema Dk Kihaule.
Aidha alisisitiza wananchi ambao tayari wamepata namba kuhakikisha wanakwenda kusajili laini zao kwa alama za vidole kabla muda haujaisha.
“Kuna watu tayari wana namba za NIDA bado hawajaenda kusajili laini za simu, kwa hiyo nawaomba wale wote wenye namba waende kusajili laini zao,”alisema Mkurugenzi huyo wa NIDA.
Mei mwaka jana Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) ilitangaza kuanza kwa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole na kuweka kitambulisho cha Taifa kama kigezo muhimu.
Mwisho wa usajili huo ulikuwa ni Disemba 31 mwaka jana, kabla ya hivi karibuni Dk. John Magufuli hajaongeza siku 20 kuanzia Januari Mosi hadi 20 mwaka huu.
Umuhimu wa kitambulisho cha Uraia umekuwa ni mkubwa kutokana na kuhitajika katika michakato mbalimbali.
Maeneo mengine ambayo bila kitambulisho cha taifa huwezi kupata huduma ni pamoja na upatikanaji wa Pasipoti (Hati ya Kusafiria).
Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nayo imeweka kigezo kimojawapo ambacho mwanafunzi anahitajika kuwasilisha ili aweze kupata mkopo ni Kitambulisho cha Taifa.
Sehemu nyingine zinazohitaji vitambulisho ni wakati wa usajili wa kampuni kwa Wakala wa usalili wa Kampuni (BRELA), Kupata leseni ya udereva, umiliki wa ardhi na hata ajira katika baadhi ya makampuni ya sekta binafsi
Pia Sekretarieti ya ajira iliwahi kutoa tangazo la ajira na kuweka kigezo kimojawapo kwa waombaji wa ajira ni kuwa na kitambulisho cha Taifa.
Tangazo hilo lilieleza kwamba kutokana na mabadiliko yaliyofanywa katika mfumo wa ajira nchini waombaji walitaarifiwa kuwa kuanzia mwishoni mwa Septemba mwaka 2019 kuwa na vitambulisho vya Taifa.
Katika kuonyesha umuhimu wa kitambulisho hicho pia mwaka jana Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma alielekeza mahakama zote nchini kutoa dhamana kwa mshitakiwa mwenye Kitambulisho cha Taifa au wenye vitambulisho hivyo kuwadhamini watu ambao kesi zao zinadhaminika.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Jaji Mkuu kutoa mapendekezo hayo kwani Julai 19 mwaka jana wakati wa mahafali ya 60 ya mawakili wapya katika shule ya Sheria Jaji Mkuu alitoa mapendekezo hay ya kutumia kitambulisho cha Taifa.
Wakati sasa akizielekeza Mahakama kuanza kutumia vitambulisho hivyo, wakati huo alipendekeza kitambulisho hicho kitumike kwenye dhamana pasipo kutaka mshitakiwa kuonyesha mali.
Pendekezo hilo alilitoa ikiwa ni katika kushauri namna ya kutatua changamoto ya msongamano wa mahabusu magerezani kwa kulegeza mashariti ya dhamana.