Unapoanza Penzi Jipya Jitahidi Kuchunguza Tabia Usikimbilie Kutaka uchi
0
January 21, 2020
Habari ya muda huu msomaji wangu. Ni siku nyingine ninakukaribisha katika ukurasa wetu wa mahusiano.
Kuna baadhi ya watu ambao wanataka kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi akisha mpenda mtu wake huambiana wachunguzane kwanza.
Ni jambo nzuri mkianza kuchunguzana ili kufahamu tabia zake japo huwezi kuzitambua zote lakini kuna baadhi utazijua.
Vitu ambavyo wengi huvikosea ni pale wanapoingia kwenye mahusiano na mtu ambaye hawafahamiani vizuri hapo unajiharibia.
Mwingine hata hujamjua vizuri ama mna siku ya tatu tayari unakimbilia kutaka mpeane mapenzi. Mnakosea sana ni vizuri kuchunguzana japo hakuna muda maalum lakini baada ya muda mtajuana vizuri baadhi ya tabia.
Jitahidi kimjua kama ni mwanamke wako ujue anaishi wapi, je ni vipi gani huwa havipendi, ni kipi anapendelea, je ameshavunja mahusiano yake ya awali. Jitahidi kufuatili ujue kiundani tabia zake.
Katika suala la tabia mwanzoni watu wengi huwa wanaficha mno makucha yao. Si rahisi sana kumjua mtu tabia yake mapema. Anaweza akawa na wewe kwa muda mrefu usimjue tabia yake mbaya. Anaweza akakuficha, akajifanya ‘malaika’, yaani mtu mwema mno kumbe nyuma ya pazia ni muuaji.
Unakuta ni mtu hatari sana asiyefaa kabisa kwenye jamii, lakini wewe ndiye umekutana naye na kuanzisha naye uhusiano. Lazima mtu kama huyo umjue kupitia mazingira yake anayoishi, watu wanaomzunguka na hata ndugu zake.
Mtu mwema lazima atakuwa na marafiki wema. Mtu mbaya, marafiki zake pia watakuwa wabaya hivyo kwa muda mfupi tu, utaweza kumjua mtu wako ni wa aina gani. Ana marafiki wema au wabaya? Familia yake ikoje?
Wakati mwingine hili jambo si rahisi sana kulijua kwa macho ya kawaida. Inabidi pia kwa imani yako umuombe Mungu akuonyeshe mtu sahihi, mtu ambaye hawezi kuwa na madhara kwako. Mwambie Mungu wako, macho yako hayaoni, lakini yeye ndiye muweza wa yote.
Akuoneshe chaguo sahihi la moyo wako. Mtu ambaye hatakusumbua kwa mambo mabaya. Mtakayesikilizana, mtakayepanga na kutengeneza maisha kama mke na mume. Hilo kwa Mungu linawezekana. Atakuepusha na wale watu hatari kwenye maisha yako.
Lakini pamoja na hayo yote, nirudi kwenye msingi wa hoja yangu. Katika hatua ya kuchunguza, unashauriwa usiwe mtu wa kuchukua muda mrefu sana. Au mtu wa kuchaguachagua sana. Huwezi kuwamaliza kama utaamua kuwachunguza wapenzi kila siku.
Unaweza kumuona huyu anapenda sana kukasirika, ukasema hafai. Huyu ni mtu wa kufuatilia sana mambo yako, naye unamuona hafai. Mwingine ana tabia ya kuchunguza sana simu yako, hapendi kukupa nafasi na marafiki zako, naye unamuona hakufai kwenye maisha yako.
Mwingine anafuatilia hadi safari zako za siku, anataka kila muda ajue upo wapi na unafanya nini. Hapendi kukuona na marafiki wa aina fulani, ana wivu wa kupitiliza hivyo unaamua kuachana naye ili uwe huru. Haya mambo yapo sana na tunayashuhudia kila kukicha kwenye jamii zetu.
Ndugu zangu, kinachotakiwa hapa si kuchagua sana. Huwezi kumpata mtu ambaye atakuwa anaendana na matakwa yako kwa asilimia mia moja. Zaidi utaambulia asilimia 50 kama si 60. Hizo 40 ni za kuzifanyia kazi mnapokuwa pamoja ili muweze kwenda sawa.
Usihangaike kumsaka mkamilifu. Utahangaika sana. Chukua muda wako kumfanya aweze kuwa sawa na wewe. Busara iwaongoze katika kung’amua mambo yenu. Ninyi wawili kupitia akili alizowapa Mungu, mnaweza kuwekana sawa na maisha yakaendelea.
Muhimu fanya uamuzi sahihi katika wakati sahihi. Usisikilize kelele za watu maana wakati mwingine wanaweza kukutoa kwenye mstari. Amua wewe na moyo wako kwamba fulani anafaa, jiridhishe, unaweza kuanzisha naye uhusiano? Basi anzeni na mumuombe Mungu awasaidie
Tags