Moshi. Waumini wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God (E.A.G.T), lililopo Soweto Manispaa ya Moshi wamepiga kambi katika kanisa hilo kupinga amri ya Baraza la Ardhi la Wilaya ya Moshi, kutaka mchungaji wa kanisa hilo, Frank Mushi kuondolewa katika nyumba ya kanisa.
Waumini hao wamepiga kambi kanisani hapo tangu Januari 6, mwaka huu wakipinga kuondolewa kwa mchungaji huyo ambaye walidai ndiye mwanzilishi wa kanisa.
Akizungumza na Mwananchi mmoja wa waumini hao Esther Lyatuu alisema Baraza la Ardhi halina mamlaka ya kumuondoa mchungaji huyo kwa matakwa ya kikundi cha watu.
Alidai hatua ya kumuondoa mchungaji ni matakwa ya baadhi ya viongozi wa juu wa kanisa hilo ambao wanajiita wadhamini.
“Sisi tumeweka kambi hapa na sasa ni wiki moja imepita tukisali ili kupinga hatua zilizochukuliwa na viongozi wa juu kumpeleka mchungaji wetu mahakamani na baadaye kumtolea vitu vyake nje,” alisema.
Akielezea tukio hilo shemasi na msimamizi wa mali za kanisa hilo, Moses Jonas alisema Januari 6 mwaka huu walikwenda watu waliojitambulisha ni mawakili wa mahakama na kuanza kutoa vitu vya mchungaji nje.
Alisema watu hao walidai mchungaji hatakiwi kukaa katika nyumba hiyo wala kuabudu kanisa hilo.
“Wadhamini wa kanisa walitaka mchungaji aende chuo cha biblia, ili awe mchungaji wa kanisa hilo kwa kuwa mchungaji wetu umri umeenda na anaumwa lakini alishindwa kufanya hivyo ndipo viongozi wa juu wakaamua kumpeleka mahakamani,” alieleza Jonas.
Jonas alisema kwamba iwapo mahakama imeamua hivyo wao hawamtaki mchungaji mwingine zaidi ya mchungaji Mushi ambaye vitu vyake vimeondolewa na waliahidi kuvilinda hadi watakapopata mwafaka.
Upendo Frank, muumuni wa kanisa hilo alisema watu wanagombania mali za kanisa hilo ni hao wanaojiita wadhamini wa kanisa la E.A.G.T, lakini hawajawahi kuwaona wakichangia chochote wala kutoa msaada katika kanisa hilo.
Alisema wanashangaa watu hao kumwondoa mchungaji ambaye amejenga kanisa na nyumba kwa nguvu zake na waumini wa kanisa hilo.
“Sisi waumini ndio tuliojenga kanisa kwa nguvu zetu pamoja na mchungaji wetu ambaye amekuwa akituongoza vyema sasa wameona kanisa limejengwa na limekuwa zuri wanamwondoa mchungaji...hatutatoa ushirikiano kwa mchungaji mwingine na tunamtaka yeye tu,” alisisiitza Upendo.