Idara ya Uhamiaji Mkoani Kagera inawashikilia watu wawili mmoja akiwa ni Raia kutoka nchini Uganda na Mtanzania mmoja kwa tuhuma za kughushi nyaraka za kujisajili ili kupatiwa kitambulisho cha Taifa, katika harakati za kufanikisha zoezi linaondelea hapa nchini la kukamilisha usajili wa laini za simu kwa alama za vidole.
Kwa mujibu wa Kamishna msaidizi Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kagera ACI Pendo C. Buteng'e amesema Tukio hilo limetokea Mnamo Januari 06, 2019 likiwahusisha Watu wawili ambao amewataja kuwa ni Frank Mpuuga (Raia kutoka Uganda), ambae amekuwa akishirikiana na Mwenyeji wake Mtanzania aitwae Swalehe Abasi Athumani Mkazi wa Mutukula Wilayani Missenyi, kughushi Nyaraka mbalimbali zikiwemo kitambulisho cha Taifa ili kuweza kukamilisha Usajili wa laini za simu kwa alama za vidole.
Afande Buteng'e ameongeza kuwa kukamatwa kwa Watuhumiwa hao kumetokana na taarifa za kiiterenjesia zilizoonesha Mtuhumiwa Frank Mpuuga kuwa na cheti cha kiapo cha wakili, akiwa tayari amekwisha jisajili NIDA kwa jina tofauti, akiwa ameingia Nchini kwa kutumia Hati ya kusafiria ya Nchini Uganda, baada ya kuhojiwa amemtaja Swalehe Athumani (mkazi wa Mutukula) kuwa ndie aliyekuwa akishirikiana nae ili kuweza kufanikisha zoezi la Vitambulisho vya Taifa na usajili wa laini za simu kwa alama za vidole.
Aidha Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti amewasihi Wanakagera waishio maeneo ya mipaka kuwafichua wale wote wanaotaka kughushi, na kufanya Udanganyifu wa aina yoyote ile ili kujipatia Vitambulisho, na kusisitiza hatua Kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao pamoja na Raia kutoka Nchi za jirani kuzunguka Mkoa Kagera wanaoshirikiana nao akiongeza kuwa wathumiwa waliokamatwa watakuwa mfano kwa wengine.