WATUMIAJI wa simu za mkononi nchini wamepokea habari njema kuwa kampuni mbili za mawasiliano ya simu za mkononi nchini za Tigo na Zantel sasa zimekamilisha zoezi la kuunganisha shughuli zao na kuwahudumia Watanzania kwa pamoja.
Katika siku za hivi karibuni, ukuaji wa mtandao wa intaneti na ongezeko la watumiaji wa simu za mkononi vimeifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika sekta ya mawasiliano kwa bara la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara. Tangazo la siku za karibuni kuwa Tigo na Zantel sasa zimeungana rasmi ni habari njema sana kwa sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi nchini Tanzania.
Japo inawezekana Watanzania wengi wanayo taarifa hii ya kuungana kwa kampuni hizo mbili, inawezekana kabisa pia kwamba wateja wengi hawafahamu nini hasa maana ya muungano huo kwao wao wateja.
Mojawapo ya faida kubwa ya msingi kwa wateja itakayotokana na muungano huu ni kwamba muda si mrefu wateja watakuwa na uwezo wa kupata huduma zote bora ambazo sasa zinatolewa na kampuni hizo mbili za simu, kila moja kivyake. Maana yake ni kwamba kama kuna huduma nzuri ya bando kwa bei nzuri Tigo basi mteja ataipata na kama kuna huduma nzuri zaidi ya muda wa maongezi Zantel basi mteja huyo pia ataipata, maana yake atanufaika na vyote vilivyo bora ambavyo sasa vinatolewa na kila kampuni kivyake.
Mbali na hilo, kampuni hizo zitanufaisha zaidi wateja na wafanyabiashara kwa kuwezesha Tigo na Zantel kutanua zaidi wigo na kuwekeza zaidi ili kuwapa wateja huduma bora zaidi na wakati huo huo kusukuma mbele gurudumu la ukuaji wa teknolojia nchini. Hapa pia tutaona ukuaji wa ubunifu wa kiteknolojia ambao kwa ujumla utaleta manufaa zaidi kwa mteja.
Katika kuleta shughuli zake za kiutendaji pamoja, kampuni hizi mbili zitaweza kuwapa Watanzania kilicho bora zaidi kwa kuruhusu fedha zaidi kutumika katika kuboresha miundombinu ya mtandao na intaneti ya kasi zaidi ya 4G. Sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi nchini ilianza kupunguza makampuni sokoni (ambayo wataalamu wameeleza kuwa uwepo wa kampuni unakuza ubora wa soko, huduma na una tija zaidi kwa wateja) wakati kampuni ya Smart Technologies ilipojiondoa na kubaki kampuni sita.
Habari hii ya karibuni ya kuungana kwa Tigo na Zantel inafanya soko kubaki na kampuni tano - namba ambayo kama inavyoelezwa na wataalamu ina tija kwa uwekezaji imara wa miundombinu ya mawasiliano ya simu na kwa ujumla faida zaidi kwa mtumiaji wa simu.
Kuja pamoja wa Tigo na Zantel ni jambo muafaka na wakati sahihi na kwa hakika itawezesha wateja kupata huduma bora zaidi huku sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi ikiendelea kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu kwa miaka mingi mbele.