Wauza Majeneza Wasababisha Msongo wa Mawazo kwa Wagonjwa


WAFANYABIASHARA ya kuuza majeneza karibu na maeneo ya hospitali wamepewa hadi Machi kuondoa bidhaa zao karibu na hospitali moja iliyopo mjini Lusaka, Zambia, kulingana na gazeti la Daily Mail.
Meya wa Mji wa Lusaka Miles Sampa amesema kwamba wauza majeneza watahamishwa hadi maeneo ya makaburini iwapo hawataondoka.
 

Wafanyabiashara hao walikuwa wamefungua maduka yao nje ya Hospitali ya Chuo Kikuu, ambapo kuna chumba cha kuhifadhi maiti. Inasemekana kwamba wagonjwa na jamaa zao waliwasilisha malalamishi yao katika mamlaka ya eneo, na kusababisha kuchukuliwa kwa hatua hiyo.

 

Meya Sampa alinukuliwa na gazeti la Daily Mail akisema kwamba wauzaji majeneza walikuwa wanawapa wagonjwa msongo wa mawazo, na kufanya iwe vigumu kwao kupata nafuu. Meya huyo pia amesema kwamba wafanyabiashara hao wameombwa kutafuta eneo mbadala la kuuza majeneza yao au wahamishwe hadi maeneo ya makaburini kuendeleza biashara yao.

 

Kwa kipindi kirefu biashara hiyo imekuwa kama mkombozi na kuwa moja ya njia kuu ya kuwapa vijana kipato na pia kuwekwa kwa majeneza hayo hospitalini, kulionekana kama eneo sahihi la kuendesha biashara hiyo. Biashara hiyo ilionekana kuhudumia zaidi wale wanaotoka maeneo ya mbali.

 

Wafanyabiashara ya kuuza majeneza pia wamekuwa wakitoa huduma nyingine kama kutayarisha mwili na kuusafirisha na kuonekana kupunguza mzigo kwa waombolezaji ambao mara nyingi huwa katika hali ya kukosa ujasiri wa kujifanyia shughuli za kumuaga marehemu.

 

Hata hivyo, biashara hiyo imekuwa ikitekelezwa karibu sana na wadi za wagonjwa ambao wamelalamika kwamba tukio hilo huwakosesha imani ya kupona hasa pale waombelezaji wanapojitokeza mchana mzima husababisha wagonjwa kufikiria zaidi kuhusu kifo badala ya uponaji.

 

Katika eneo hilo kifo kimekuwa kikichukuliwa kama biashara nyingine yoyote, mfano uuzaji wa dawa na kadhalika. Wakazi wanaamini kwamba majeneza hayastahili kuuzwa kwenye hospitali hiyo kwa sababu hilo ni eneo linalostahili kuwapa wagonjwa moyo na utulivu wa akili badala ya kuwatia hofu.

 



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad