KIKOSI cha Yanga leo kitashuka dimbani kusaka pointi tatu dhidi ya Singida United, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Namfua, Singida.
Yanga itaikabili Singida, ikiwa na hasira za kupoteza mechi mbili mfululizo zilizopita, ikianza kubamizwa mabao mabao 3-0 na Kagera Sugar 3-0, kabla ya kuchapwa bao 1-0 na Azam FC 1-0, michezo yote ikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hiyo itaingia uwanjani kusaka ushindi kwa sababu mbili, kwanza kumaliza hasira za kupoteza michezo hiyo miwili iliyopita, lakini kupunguza pengo la pointi kati yao na watani zao, Simba walio kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Yanga inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi 25, baada ya kucheza michezo 14, ikishinda saba, sare nne na kupoteza tatu, ikiwa nyuma kwa pointi 16 dhidi ya Simba iliyocheza michezo 16 hadi sasa.
Singida kwa upande mwingine, inashika nafasi ya 19 ikiwa na pointi 10, baada ya kucheza michezo 16, ikishinda miwili, sare nne na kupoteza 10.
Itaikabili Yanga, ikiwa na morali ya hali juu inayotokana na kutoka kuvuna ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting, katika mchezo wao uliopita uliochezwa kwenye uwanja huo.
Mchezo huo ni mtihani mwingine kwa kocha wa kikosi cha Yanga, Luc Eymael ambaye tangu achukue mikoba ya kuliongoza jahazi hilo, hajafanikiwa kuvuna ushindi katika michezo miwili iliyopita.
Kikosi cha Yanga chini ya Eymael hakijafanikiwa kufunga bao, huku pia kikiruhusu wavu wao kutikiswa mara nne, wastani wa kufungwa mabao mawili kila mchezo.