Viongozi wa Klabu ya Yanga wameafikiana kuachana na Mshambuliaji David Molinga aliyekuwa akiichezea klabu hiyo kwa mkopo na kusajili wachezaji wengine wanaoamini wataisaidia timu hiyo kwa nidhamu ya hali ya juu
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema, wapo kwenye mazungumzo ya kuvunja mkataba na Molinga aliyeshindwa kufikia malengo kwa mujibu wa mkataba wake wa miaka miwili akitokea kwao, DR Congo
Amesema, “Mbadala wa Molinga atajulikana kwani bado tuna nafasi na tunaendelea kusaka mchezaji anayeweza kuwa msaada kwenye kikosi chetu ambacho kinahitaji maboresho kabla ya dirisha kufungwa.”
Molinga aliyetibuana na viongozi kwa kitendo alichokionesha alipofanyiwa mabadiliko katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara, amekuwa ni mchezaji wa tano aliyesajiliwa na Kocha Mwinyi Zahera kutimka Jangwani
Wachezaji wengine waliosajiliwa na Zahera waliondoka ni Sadney Urikhob, Juma Balinya, Issa Bigirimana na Maybin Kalengo. Molinga anaondoka akiwa kinara wa ufungaji wa Yanga katika Ligi Kuu Bara akiwa na magoli manne