AMETOSWA! Licha ya kupigania kwa udi na uvumba mali za aliyekuwa mumewe Ivan Ssemwanga, staa wa Afrika Mashariki, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, kwa mara nyingine ametoswa kumiliki baadhi ya mali hizo, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limeidaka. Hatua hiyo imekuja baada ya ukoo wa Tycoon Ivan aliyekuwa maarufu kama ‘Don Ivan’ (40), kumteua mtoto mkubwa wa Zari na Ivan, Pinto Ntale kurithi mali za baba yake zilizopo huko nchini Uganda.
Ni sawa na kusema Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya wa 2020 hazikumwendea poa mwanamama huyo ambaye pia amezaa watoto wawili na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ baada ya kikao cha familia kutoa uamuzi huo mzito.
MCHAKATO ULIVYOANZA
Wiki iliyopita, Zari pamoja na watoto wake wawili, Raphael Junior na LilQ Quincy walipaa kutoka Afrika Kusini kuelekea Uganda na kumwacha mtoto mkubwa, Pinto ambaye inaelezwa kuwa vielelezo vyake vya safari vilizuiwa na idara ya uhamiaji nchini humo.
Baada ya kuwasili nchini Uganda, familia ya Ssemwanga iliketi na kumtaja mmiliki halali wa mali za marehemu Ivan zilizopo nchini Uganda kuwa ni Pinto kwa kuwa sasa ametimiza umri wa utu uzima kwa kuvuka miaka 18. Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari nchini humo, uamuzi huo ulitolewa katika kikao hicho cha kifamilia kilichofanyika nyumbani kwa marehemu Ivan katika Kijiji cha Kayunga Wilaya ya Nakaliro, Uganda.k
Akizungumza na wanahabari, mjomba wa Pinto alisema; “Watu wote waliokuja hapa leo wanatuona tunamfanya Pinto kuwa mrithi rasmi wa Ivan Ssemwanga, napenda kumuagiza Dido achukue picha ya kaka yake, Pinto kwani ukoo wote unamkubali kama mrithi wa kweli wa baba yake.”
Aidha, alipokuwa nchini Uganda, mama huyo wa watoto watano alibandika picha alizopiga na magari yake ya kifahari yakiwemo Mercedes Benz, Chrysler na Hummer H3 ambayo yote yamebandikwa ‘plate’ namba zenye jina lake. Pia alitupia picha za jumba kubwa la kifahari analomiliki nchini Uganda.
KWANINI AMETOSWA
Itakumbukwa kuwa, miezi miwili baada ya Ivan kufariki dunia Mei 25, mwaka 2017 na kuzikwa Mei 30, mwaka huohuo, baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa baadhi ya mali zake zilizopo nchini Uganda ni pamoja na majumba kadhaa ya kifahari, viwanja, na magari, jambo ambalo Zari aliibuka na kukanusha baadhi ya mali hizo.
Zari aliibuka na kuweka wazi kuwa moja ya majumba hayo ambayo aliweka picha zake mtandaoni kuwa haijawahi kumilikiwa na Ivan kama ‘blogi’ zilivyosema. Aliendelea kusema kwamba aliijenga nyumba hiyo na pesa zake, hivyo wenye wivu ndiyo wanaomzushia kuwa siyo mali zake.
“Ukweli ni kwamba, sikuwahi kurithi nyumba hii. Haikuwahi kuwa ya Ivan. Niliijenga hii mwenyewe kutoka mwanzo! Hamuwezi kuzuia mafanikio ya mtu. Huo ni ujinga,” aliandika Zari kwenye Instagram. Hata hivyo, siku chache kabla Ivan hajafariki dunia, Zari alizozana na Lawrence Kiyingi maarufu kama King Lawrence aliyekuwa rafiki wa karibu wa Ivan kuhusu mali za mumewe.
Ivan ambaye alikaa katika chumba cha uangalizi maalum kwa muda wa wiki mbili, baada ya kifo chake, Zari aliamuru madaktari wasitangaze kwanza kuhusu kifo hicho hadi hapo atakapokusanya mali za marehemu na kuzihamishia sehemu nyingine.
Hata hivyo, King Lawrence ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Ivan na pia mwanachama wa Kundi la Rich Gang ambalo ni maarufu nchini Uganda kwa kuandaa na ‘ku-host’ shoo za nguvu, baadaye aliteuliwa kuwa msimamizi wa baadhi ya mali za marehemu, jambo ambalo lilizidi kumuumiza Zari.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa familia na marafiki wa Ivan walikuwa wakimpiga vita Zari kwa maazimio yake ya kutaka kurithi mali zote za aliyekuwa mumewe, jambo ambalo sasa linaonekana kufanikiwa. Zari kwa sasa ndiye msimamizi mkuu wa shule zaidi ya 30 na Chuo cha Brooklyn vilivyopo Afrika Kusini pamoja na nyumba za kukodisha.
GPL