Ado Shaibu achukua fomu kugombea Ukatibu mkuu ACT Wazalendo




Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma Ado Shaibu atangaza nia ya kugombea nafasi ya katibu mkuu wa ACT Wazalendo na kuamua kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.

Ado amesema nafasi ya ukatibu mkuu katika chama chao ni lazima uchukue fomu na kuchaguliwa kwakuwa anahitaji Katibu Mkuu ambaye atakifanya Chama kiendeshwe kwa kasi na ufanisi mkubwa huku akiimarisha mshikamano, umoja na upendo ndani ya Chama na ndani ya nchi.

"Binafsi nimefarijika kuona tayari wanachama wawili, Ndugu Dorothy Semu na Ndugu Joran Bashange wamechukua fomu za kuwania nafasi hii. Wote wawili ninawafahamu vyema na ni watu ninaowaheshimu. Nina imani sisi watatu, iwapo tutateuliwa kuwa wagombea, tutaipa Halmashauri Kuu fursa ya kipekee ya kuchagua Katibu Mkuu bora anayeendana na wakati tunaoishi".

Hivi sasa, Chama chetu na nchi yetu kwa ujumla, vinapitia kwenye kipindi cha kipekee sana. Kipindi hiki, pasi shaka,  kinahitaji Katibu Mkuu wa kipekee pia.

Tunaishi katika zama ambazo CCM na Serikali yake inawahofia viongozi wetu wakuu kupita kiasi na wamepanga njama mara kadhaa kuwafungia kisiasa, kufuta Chama, kuwabambikia kesi zisizo na dhamana na ikibidi kuwaua. Tunamuhitaji Katibu Mkuu atayeielewa hali hii vizuri na atayekilinda Chama chetu kwa wivu mkubwa. 

Tunaishi katika zama ambazo CCM inahofia sana uchaguzi na inatamani kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kurudia uhuni walioufanya  kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tunahitaji Katibu Mkuu ambaye atafahamu kuwa huu ni mwaka wa maamuzi na hivyobasi yeye mwenyewe kuongoza programu za kuongoza umma kudhibiti uhuni huo. 

Tunaishi katika zama za Serikali iliyovuruga kupindukia uchumi wa nchi yetu na kusababisha hali mbaya ya maisha ya Watanzania. Tunahitaji Katibu Mkuu ambaye atafahamu wajibu wa Chama chetu katika kuwahamasisha, kuwaunganisha na kuwaongoza Watanzania katika kuing'oa CCM ili kuunusuru uchumi wa nchi na kukata minyororo ya unyonyaji na ukandamizaji. 

Tunaishi katika zama ambazo CCM imeonesha mapema kushindwa huko Zanzibar. Kila njama wanayofanya inagonga ukuta.  Tunahitaji Katibu Mkuu ambaye ataelewa nafasi ya kipekee na ya  kihistoria ya Chama chetu katika kuhitimisha safari ndefu ya mapambano ya Wazanzibari katika kujikomboa.

Tunaishi katika zama za ukandamizwaji mkubwa wa haki za binadamu hapa nchini. Watu kuuawa, kutekwa na kubambikiwa kesi limekuwa jambo la kawaida. Vyama vya siasa, Asasi za Kiraia, makampuni binafsi, wafanyabiashara, taasisi za uwajibikaji na wananchi kwa ujumla wameguswa na utawala wa kimabavu wa Serikali ya Awamu ya Tano. Tunahitaji Katibu Mkuu ambaye ataendeleza kwa kasi nafasi ya Chama hiki kama "Sauti ya Wasio na Sauti".

Tunaishi katika zama ambazo Watanzania wana kiu kubwa ya mabadiliko na wameonesha mapenzi makubwa kwa Chama chetu kama mbadala wa uhakika.   Tunahitaji Katibu Mkuu ambaye ataongoza jitihada za kuwafikia wananchi kwenye kila kona ya nchi ili waingie kwenye jahazi la Wazalendo. 

Wakati utapofika, kama nitafanikiwa kuteuliwa kuwa mgombea, nitaeleza kwa kina namna nilivyojipanga kuwa Katibu Mkuu bora na wa viwango kuendana na hali ya sasa. Kwa kuzingatia hoja hizo, na kwa kuwapima wenzangu, Dorothy Semu na Joran Bashange (na wengine wataojitokeza), nina imani kuwa Halmashauri Kuu ya Chama itapata fursa muafaka ya kuchagua Katibu Mkuu anayefaa. 

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad