Ni kweli, wakati mwingine hatuelewi utamu wa madaraka, wala uzuri wake na hata wakati mwingine hatuelewi chochote kuhusu madaraka, tunayapokea kutokana na utofauti wa tabia zetu za kuzaliwa, au ndivyo yalivyo.
Nilimkumbuka Tolstoy baada ya juzi kumuona Waziri Mkuu wangu wa zamani, Fredrick Sumaye akiingia ofisi ndogo za chama chake cha zamani cha Mapinduzi (CCM), pale Lumumba alipotangaza rasmi kurudi kundini.
Kando yake walikuwepo makada wengine sambamba na vijana wapya waliojiunga na chama hicho.
Sumaye alikuwa akipiga makofi pale nyimbo kadhaa za kusifu chama hicho zilipokuwa zikiimbwa. Moyoni nilijisemea, ‘Labda hatimaye amekubali’.
Ndiyo, labda amekubali kwamba haina haja ya kujihangaisha sana na siasa. Haina haja ya kubaki upinzani. Hakuna haja ya kuwa mbali na chama chake ambacho kiliwahi kumpatia uwaziri mkuu wa nchi hii.
Si mawaziri wakuu wote waliokaa madarakani miaka 10 hapa nchini, lakini Sumaye alikaa siku ya kwanza mpaka ya mwisho.
Aliondoka kwenye nafasi hiyo akiwa na umri wa miaka 55. Alijaribu bahati yake ya kutaka apatiwe ridhaa ya kushika cheo cha juu zaidi nchini cha Urais, lakini nyota ya mwanasiasa anayeitwa Jakaya Mrisho Kikwete ilikuwa iking’aa zaidi kwa wakati huo ambao Sumaye pia alijaribu bahati yake.
Baada ya hapo, ilitazamiwa kwamba Sumaye angenyoosha mikono juu. Mioyo yetu ilimruhusu kwa wakati ule kujaribu bahati yake ya kuwania Urais. Kama tulivyofanya miaka 10 baadaye, tulimruhusu Mizengo Pinda kuwania Urais baada ya kipindi chake cha Uwaziri mkuu kumalizika.
Sumaye alipokosa kipindi kile, tulijua angeingia katika mkumbo wa Mawaziri wastaafu walioamua kusahau ndoto ya kuwa Marais wa nchi hii, kumbe haikuwa hivyo. Wapo akina Salim Ahmed Salim, John Malecela na Joseph Warioba walioamua kubakia kuwa Mawaziri wakuu wastaafu tu. Maisha hayawezi kukupa kila unachotamani. Maisha hayawezi kukupa kila kitu unachotaka. Miaka 10 baadaye, Sumaye aliamua kuachana na kapu la wastaafu waliotulia na kujitia tena katika ‘vurugu’ za siasa. “Kwa nini sasa” Wengi tulijiuliza.
Kuna wazee wetu wengi wamefariki dunia wakiwa wastaafu katika kazi za ualiamu, ulinzi wa magetini, uandishi wa habari na taaluma nyingine nyingi, lakini walifariki dunia huku mioyo yao ikiwa imeridhika na nafasi na fursa walizopata huku duniani.
Unakuaje Waziri Mkuu mstaafu, mwenye gari la serikali, posho na heshima katika jamii, lakini bado unautamani Urais katika kiwango kilichopitiliza?
Rafiki yake wa baadaye, Edward Ngoyai Lowassa alikuwa na mpango ambao ulikuwa haujakamilika (unfulfilled mission) na baada ya kuwa Waziri Mkuu kwa miaka miwili tu, tulijaribu kumuelewa katika ndoto yake ile ya Urais. Lakini Sumaye hatukuwahi kumuelewa.
Hata baada ya kulalamikia mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM na kisha kuhamia Chadema, wengi tulimuelewa Lowassa, lakini si Sumaye.
Lowassa alikuwa anataka kumalizia ndoto yake, lakini miaka miwili aliyoishia njiani kama Waziri Mkuu haikutosha kukata kiu yake ya kuitengeneza ‘Tanzania anayoitaka’. Lakini kwa Sumaye tulishangaa. Anataka nini zaidi? Tukajiuliza, baada ya kuwa nje ya madaraka makubwa aliyokuwa nayo, kwa nini asingepumzika Kibaha na kulima?
Hata mpango wake wa kwenda Chadema inadaiwa aliupanga kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kugombea nafasi ya Urais siku za usoni kama Lowassa angefeli na kuondoka katika hisia za watu.
Wakati Lowassa aliposalimu amri na kurudi nyumbani, Sumaye ndio kwanza alikuwa anagombea nafasi ya Uenyekiti wa kanda ya kati kwa chama chake cha upinzani cha Chadema.
Yaani kutoka kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania mpaka kugombea nafasi ile, Sumaye alikuwa anataka nini zaidi?
Hapa ndipo tunapomkumbuka Tolstoy. Hatuwezi kuyaelewa vema madaraka. Inawezekana ilikuwa ni njia sahihi ya kujijenga na kujipa nguvu ndani ya Chadema kiasi kwamba aaminike kugombea Urais kwa tiketi ya chama chao.
Ukweli ni kwamba, baada ya Lowassa kurudi CCM, Chadema wasingemuamini Sumaye. Walijua na yeye angerudi kundini. Lakini achilia mbali hilo, siasa za kwetu ni za kujuana zaidi. Chadema hawawezi kumuamini mtu mwingine nje ya kundi lao ambalo limewahi kupigwa virungu na polisi na kupata mateso ya hapa na pale.
Inawezekana kila walipokuwa wanatazamana walikuwa wanaangaliana zaidi kwa historia ya wapi walitoka, ni makovu mangapi wameyapata pamoja, ni damu lita ngapi walimwaga pamoja. Hawakuona kama Sumaye ni mwenzao. Yeye na Lowassa ni watu waliochukuliwa njiani tu kama karata ya papo kwa hapo ya kisiasa, lakini si ya mpango wa muda mrefu.
Haikushangaza kuona Chadema kwa nini hawakushtuka Lowassa aliporudi kundini kule Lumumba na wala sasa hawajashangaa kuona Sumaye amerejea Lumumba.
Waliwachukua kwa karata ya mwaka 2015. Ndivyo Freeman Mbowe na watu wake walivyo. Ndivyo siasa ilivyo.
Tunachojiuliza ni je amekubali kuwa sasa analazimika kubakia katika historia tu kuwa ni Waziri Mkuu wetu wa zamani? Kama amekubali, hili litakuwa jambo la maana. Kitu cha kwanza amejisaidia yeye mwenyewe na familia yake. kwa nini apate bughudha zisizo za msingi za hali na mali?
Kwa nini watoto na wajukuu wasumbuke bila sababu za msingi? CCM wana utaratibu wao wamejiwekea katika suala la Rais aliyepo madarakani kukaa miaka 10.
Mei 29, mwaka huu, Sumaye atatimiza umri wa miaka 70. Kwa nini aendelee kuota ndoto isiyowezekana? Awe mgombea wao akiwa na umri wa miaka 75? Sidhani.
Lakini Sumaye pia ameisaidia CCM. Sio kwamba walikuwa na hofu naye kwa kuwapo upinzani, hapana, lakini walikuwa wanamtazama kwa jicho la aibu. Yeye na Freeman Mbowe hawawezi kufanyiwa ubaya wa aina moja. Kwa itifaki, Sumaye alifika nafasi za juu. Soni lazima iwepo. Vyovyote ilivyo Sumaye amechukua uamuzi wa msingi. amechukua uamuzi kama aliouchukua Lowassa, lakini nadhani yeye amechelewa kidogo.
Baada ya upepo wa uchaguzi wa ndani ya chama kumalizika, asingesubiri hadi aaibishwe na Chadema kwa kukosa nafasi ya Uenyekiti wa kanda wakati tayari alishakuwa Waziri Mkuu wa nchi hii.
Shida ni kuwa alikuwa ‘akiendesha gari lake’ kwa mwendo wa kasi bila kujua safari anayokwenda. Kwa sasa afadhali ameweka gia ya ‘rivasi’ na amerudi kule alikotoka. Ni maamuzi sahihi. Watanzania wachache watapinga maamuzi yake. sidhani kama wanaopinga maamuzi yake wanaweza kujaza ukumbi wa Diamond Jubilee