Aunt afunguka skendo ya fumanizi



HABARI kubwa wikiendi iliyopita ni skendo ya fumanizi matata lililofanywa na staa wa sinema za Kibongo, Aunt Ezekiel.  Kwa mujibu wa kurasa za udaku kwenye Instagram, Aunt alimfumania mumewe, Moses Iyobo na muandaaji wa Shindano la Miss Kinondoni, Nancy Joseph maeneo ya Kinondoni jijini Dar na kuzichapa kavukavu. Kufuatia habari hizo, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limekaa kitako na Aunt na kumtaka kueleza kile anachokijua juu ya tukio hilo, ambapo alifunguka.

Aunt amesema hana muda mchafu wa kupigana na mtu. Amesema anachokijua ni kwamba, kuna watu wanatafuta kiki mitandaoni kupitia jina lake na ndiyo maana hata huo uzushi wa kupigana anaona ni wa kipuuzi. “Kuna wakati mtu anakuchokonoa hadi inafika mwisho, ukija kuuliza kulikoni unasikia ni mtu anatafuta kiki isiyokuwa na maana.

“Mimi siwezi kupigana na mtu yeyote,” amesema Aunt anayesemekana kwamba siku hizi anawajibu vibaya hata mashabiki wake kwenye Instagram. Aunt ameendelea kusema  kuwa, anasikia alipigana na huyo dada (Nancy) kwa ajili ya Iyobo, jambo ambalo halijawahi kutokea na hafikirii kufanya hivyo, ingawa kuna watu wanamchokoza.

“Kiukweli mtu akinichokoza nitakula naye sahani moja, lakini ishu ya kusema nimepigana, sitaki kumpa mtu kiki. “Kila mtu atafute njia ya kupata kiki na siyo kupitia migongo ya watu wengine,” amesema Aunt.

Hata hivyo, wakati Aunt akisisitiza hivyo, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limekutana na chanzo kilichoshuhudia Aunt na Nancy wakizichapa kavukavu kwenye sherehe ya kuzaliwa mpambaji maarufu aitwaye Natalia na kuzua tafrani kabla ya kutulizwa na kila mmoja kuchukua hamsini zake.

Inasemekana, wakati Aunt alipotengana na Iyobo kwa miezi kadhaa mwaka jana, Nancy ndiye aliyechukua nafasi hiyo ya Aunt na baada ya wawili hao kurudiana, ndipo uhasama kamili ukaibuka.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad