Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Akiuka Mkataba wa Kidiplomasia; Ashiriki Mikutano ya ACT-WAZALENDO Zanzibar


Kaimu Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Inmi Patterson anakiuka mkataba wa Kidiplomasia kwa kufanya mikutano ya siri na Chama cha ACT-Wazalendo Visiwani Zanzibar.

Akiwa Visiwani Zanzibar Kaimu Balozi huyo wa Marekani amefanya kikao cha siri na Mshauri wa Chama cha ACT Wazalendo, Seif Shariff Hamad ambapo mazungumzo yao hayakuwekwa bayana yalilenga katika dhamira ipi.

Taarifa kutoka ndani ya Chama cha ACT-Wazalendo zinasema kwamba, mazungumzo yao yalihusu zaidi masuala ya Uchaguzi Mkuu na namna walivyojipanga katika kushinda uchaguzi huo.

Katika kikao cha Kaimu Balozi huyo wa Marekani kilifanyika nyumbani kwa Mshauri wa ACT- Wazalendo,Seif Shariff Hamad huko Chukwani nje kidogo ya Jiji la Zanzibar saa 1:00 hadi 1:45 usiku.

Kitendo cha Kaimu Balozi huyo kwenda nyumbani kwa Seif Shariff Hamad kufanya kikao kinathibitisha dhamira mbaya kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa misingi ya maadili ya Kidiplomasia inazuia Balozi au mfanyakazi wa Ubalozi kujihusisha na masuala ya kisiasa ya nchi rafiki.

Mwanadiplomasia huyo amekuwa akilalamikiwa na watu wa kada mbalimbali kwa vitendo vyake vya kuonana na wananchi na kufanya mazungumzo yenye sura ya kisiasa wakati yeye hatakiwi kufanya vitendo hivyo kwa mujibu wa kazi iliyomleta hapa nchini.

Habari kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zinasema kwamba , Kaimu Balozi Patterson aliomba kwenda Zanzibar kukutana na raia wa Marekani,lakini cha kushangaza amekuwa akikutana na wanasiasa wa vyama vya upinzani katika mikutano ya siri.

“Aliomba kibali cha kwenda Zanzibar kukutana na raia wa Nchi yake badala yake anakutana na kufanya mazungumzo na vyama vya siasa ni dhahiri kuwa anakiuka utaratibu” kilisema chanzo cha habari kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania.

Kinyume na ruhusa aliyopewa, Kaimu Balozi huyo inaonekana wazi kuwa ameidanganya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuitumia ruhusa aliyopewa kinyume na madhumuni yake.

Ni wazi kuwa mwenendo wa Kaimu Balozi unakiuka mkataba wa Kimataifa wa uhusiano wa kidiplomasia wa Vienna wa mwaka 1961 kwa kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania na kibaya zaidi amekuwa akionesha ushabiki wa kisiasa.

Mkataba wa kimataifa Vienna unaoshughulikia uhusiano wa kidiplomasia wa Mwaka 1961 ibara ya 41(1) unakataza mabalozi na wanadiplomasia kuingilia masuala ya ndani ya nchi wenyeji na pia kutimiza wajibu wa kuheshimu kinga ya kidiplomasia.


Taarifa zaidi zinasema kuwa hii si mara ya kwanza kwa Kaimu Balozi huyo kukutana na kufanya mazungumzo ya siri na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani na haikuweza kufahamika mara moja dhamira ya kufanya hivyo.

Sheria ya Diplomasia ya Jamhuri ya Muungano waTanzania ya Mwaka 1986 ambayo ni zao la Mkataba wa Kimataifa wa uhusiano wa kidiplomasia wa Vienna hairuhusu Balozi au mfanyakazi wa Ubalozi kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi ikiwemo masuala ya kisiasa.

Source: JF
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad