BAO alilofunga mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu Morocco akiichezea klabu yake ya Difaa El Jadida liliwafanya vigogo wa Wydad Casablanca kucharuka na kutaka kumfuta kazi Kocha Sébastien Desabre.
Jumatatu ya wiki hii, zilizagaa taarifa kocha huyo aliyeiongoza Uganda katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Misri, amefutwa kazi kufuatia kipigo walichopewa Februari 15 wakiwa nyumbani kwenye uwanja wao wa Stade Mohamed V, Casablanca.
Hata hivyo, saa 24 baadaye ilitolewa taarifa kocha huyo Mfaransa ataendelea kuinoa timu hiyo, Msuva ambaye angekuwa sehemu ya kufukuzwa kwa kocha huyo alisema tetezi hizo, hazikumfurahisha.
“Nilikuwa pale kwa ajili ya kuhakikisha naisaidia timu yangu kupata ushindi, mchezo ulikuwa mgumu na walikuwa wakitushambulia sana, lakini shambulio la kushtukiza ndilo tulilolitumia kuwafunga.
“Kocha wao namjua vizuri. Ningejisikia vibaya kuwa sehemu ya kufukuzwa kwake, binafsi namtakia kila la heri katika michezo iliyopo mbele yake, ana presha kubwa kwa sasa kwa sababu Wydad Casablanca ni timu kubwa ambayo kila siku inahitaji na matokeo mazuri,” alisema Msuva.
Kwa mujibu wa Rais wa klabu hiyo, Said Naciri alinukuliwa na mtandao mmoja mkubwa nchini humo akisema viongozi wenzake walichukizwa na matokeo hayo hivyo walikuwa tayari kumfuta kazi kocha huyo.