ALIYEWAHI kuwa Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Simbeye, ametangaza kuachana na chama hicho huku akidai kuwa kimekuwa kikiongozwa na kuamriwa na mtu mmoja kama kampuni binafsi na kuongeza kuwa kwa sasa anapumzika kwanza kufanya mambo ya siasa.
“Mambo ya Chadema yanatakiwa kuamuliwa kwa mujibu wa katiba, kanuni na miongozo ya chama, leo yanaamuliwa kwa kauli na amri za Mbowe. Mwenyekiti ameamua kugeuza chama kuwa mali yake binafsi, lakini tukitoka nje tunawaaminisha umma kuwa chama hiki ni mali ya Watanzania.
“Kuna mambo mengine kiungozi tunapaswa kuwa na akiba ya maneno kama ukiyasema, kunaleta madhara makubwa, tumepoteza majiji ya Dar na Arusha, bado tunawaambia Watanzania tupo imara, tunasema waende tu.
“Juzi nimeona tweet ya mjumbe wa kamati kuu anasema wanaoenda ni panya, kiongozi unaingia kwenye kikao kikubwa cha chama, unaamini anayeondoka ni panya. Chama cha siasa ni watu. Kila mtu ana haki ya kulinda utu wa mwenzie. Je, kumuita mwenzio mwanamme suruali, au panya ni sawa?” amesema Simbeye.