Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba amesema mkoa wake unaahidi kutoa Sh1 milioni kwa Rais John Magufuli kwa ajili ya kuchukulia fomu ya kugombea urais.
Kamba ameyasema hayo leo Februari 13, 2020 Jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe ya maadhimisho ya miaka 43 ya kuzaliwa kwa CCM huku Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akiwa ndiyo mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
Kamba amesema chama hicho hakina cha kumlipa Rais Magufuli kwa sababu ameufanyia makubwa mkoa wa Dar es Salaam katika mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara, hospitali na mingine mingi.
“CCM Mkoa wa Dar es Salaam tunatangaza rasmi kwamba, kwa upande wa urais, mgombea wetu ni Rais John Magufuli. Tutatoa Sh1 milioni kwa ajili ya kumchukulia fomu ya urais. Kwa hiyo, tunakuomba (Makamu wa Rais) utufikishie salamu hizi kwa Rais Magufuli, asihangaike na hela ya kuchukulia fomu, sisi tutatoa,” amesema Kamba.
Mwenyekiti huyo amesema kwa kuwa makao makuu ya nchi yamehamia Dodoma, watamkumbuka Rais Magufuli kwa kuuletea Mkoa wa Dar es Salaam maendeleo makubwa ambayo yataufanya kuwa kitovu cha biashara hapa nchini.
Wakati huohuo, Kamba amesema chama hicho kitatoa Sh100 milioni kwa ajili ya kuimarisha mashina ya chama hicho, amesisitiza kwamba fedha hizo ziko tayari na zitaanza kutolewa baada ya utaratibu unaoandaliwa kukamilika.