Mtoto mchanga nchini China ameambukizwa virusi vya corona saa 30 baada ya kuzaliwa, kisa chenye kuhusisha mtoto mchanga zaidi kuwahi kurekodiwa, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.
Wauguzi wakiwa na mtoto mchanga
Mtoto alizaliwa tarehe 2 mwezi Februari katika hospitali moja ya mjini Wuhan, ulio kitovu cha mlipuko wa virusi hivyo.
Mama wa mtoto alikutwa na virusi hivyo kabla ya kujifungua. Haijulikani ni kwa namna gani kichanga hicho kiliambukizwa.
Shirika la habari la China, Xinhua limeripoti taarifa za maambukizi siku ya Jumatano.
Ilieleza kuwa mtoto aliyekuwa na uzito kilogramu 3.25, alikuwa na hali nzuri na alikuwa akifanyiwa uchunguzi.
Mtoto huambukizwa vipi?
Wataalamu wa afya wanasema inawezekana ni maambukizi yaliyotokea tumboni.
”Hii inatukumbusha kuwa makini kuwa kuna uwezekano kukawa na maambukizi ya virusi vya corona kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.” Daktari wa hospitali ya watoto kitengo cha dawa, Zeng Lingkong aliliambia shirika la habari la Reuters.
Lakini pia inawezekana mtoto aliathirika baada ya kuzaliwa na kuwa karibu na mama yake.
”Inawezekana kuwa mtoto alipata maambukizi kwa njia za kawaida- kwa kuvuta hewa iliyotoka kwa mama alipokohoa,” daktari wa magonjwa ya maambukizi Stephen Morse ameeleza.Wauguzi wakiwa na mtoto mchanga
Ni kawaida kwa watoto kupata virusi?
Watoto wachache sana wamegundulika kuwa na virusi vya corona katika mlipuko wa hivi karibuni, sawa tu na aina nyingine ya maradhi ya Sars na Mers.
Ripoti ya jarida la kitabibu limesema wastani wa umri wa wagonjwa ni kati ya miaka 49 na 56, kwa upande wa watoto ni mara ”chache sana”.
Vivyo hivyo, wakati wa mlipuko wa Mers mwaka 2016, Jarida la afya kuhusu maradhi ya watoto lilisema kuwa virusi vilikuwa vikiwaathiri watoto kwa nadra sana, hata hivyo sababu hazijulikani.
Mtoto wa miezi sita nchini Singapore aligundulika kuwa na virusi vya corona , halikadhalika mtoto wa miaka minane aligundulika kuwa na virusi hivyo mjini Wuhan, ambaye kwa sasa yuko Australia.
Virusi hivyo vimesambaa nje ya China, mataifa 25 yakithibitisha kuwa na visa 191 vya maambukizi, kumeripotiwa vifo viwili pekee nje ya China.