Kila binadamu ameumbwa na kiu ya kufanikiwa katika kila kitu anachofanya. Mafanikio ndio kilele cha mlima mkubwa wa maisha ambao umejengwa kwa misingi na ngazi za mihangaiko na mitihani ambayo unapaswa kuivuka ili upumzike kwenye kilele hicho.
Kwa bahati mbaya, unaposema ‘mafanikio’ wengi hufikiria kuhusu ‘utajiri’. Lakini ukweli ni kuwa kuna tofauti kati ya kuwa tajiri na kufanikiwa kiuchumi. Unaweza kuwa tajiri lakini ukawa bado hujafanikiwa. Kwa kuwa watu wanawaza utajiri kuwa ndio kigezo cha mafanikio hujikuta wakijiingiza kwenye vitendo vya ajabu kwa lengo la kujizolea mali lakini mwisho huwa wanagundua kuwa hawajafanikiwa japo jamii inahisi wamefanikiwa.
Nanachoamini mimi, kufanikiwa kweli ni kutimiza malengo yako kwa ufanisi na kwa wakati, lakini mafanikio hayo yakupe amani moyoni mwako (peace of mind).
Vinginevyo, utafanikiwa kwa mrundikano wa fedha huku ukitengeneza tatizo kubwa zaidi la msongo wa mawazo na ukosefu wa amani ya moyo. Hivyo, mafanikio ya njia ya mkato ni mafanikio feki yanayokuja na matatizo mengi mazito zaidi.
Kwa utangulizi huo mrefu, naamini utanielewa zaidi napokupitisha kwenye hizi ‘siri za wazi’ za mafanikio ya kweli katika maisha.
1. Jiamini
Mafanikio ya kweli yanaanza na wewe. Hivyo, kujiamini ni msingi mzuri utakaokufanya utambue uwezo wako katika kufanya jambo fulani. Amini uwezo wa kufanya jambo hilo uko mikononi mwako. Usijishushe, jipime kwa mengi mazuri unayoweza kufanya, ikatae roho ya kujiona huwezi.
2. Thubutu
Neno hili pia ni msingi wa pili mkuu wa mafanikio. Uoga wa kuthubutu ni kikwazo kikuu kinachowarudisha wengi nyuma na kujikuta hata kuanza safari ya mafanikio hawawezi. Jambo lolote zuri na kubwa huwa gumu kufanya na ni rahisi kuhisi haliwezekani. Usikubali kushindwa bila kujaribu. Thubutu kwa dhati na weka nguvu yako na akili yako yote katika uthubutu huo. Hata hivyo, katika uthubutu huu, unapaswa kupima vizuri ili uchukue ‘calculated risk’ na sio ‘just risk’.
3. Panga na tekeleza kwa vitendo
Kumbuka, ukishindwa kupanga ujue umepanga kushindwa. Kuwa na mipango inayopimika na kutekelezeka kwa kiwango cha juu. Usiwe na mipango tu mikubwa ambayo hata utekelezaji wake hauwezekani. Unapopanga fikiria wapi utapata rasilimali na jinsi ya kutelezeka, lakini pia mpango wako ukupe uwezo wa kuutathmini na kujipima mwisho wa kazi hiyo. Hata hivyo, mipango haitakuwa na maana kama hautaitekeleza kwa ufanisi. Ukishindwa kutekeleza mpango wako, rudi angalia ulipoteleza ili urekebishe na sio kuufuta mpango mzima bila sababu za msingi.
4. Tengeneza mtandao na wasiliana
Mtandao ni kama daraja au miundombinu ya kuyafikia mafanikio. Hakikisha haujifungii kwenye dunia yako peke yako. Hakikisha kila unaekutana naye na kupata nafasi ya kumfahamu kama mtu anayeweza kuwa sehemu ya daraja bora kwa namna moja au nyingine, anakuwa sehemu ya mtandao wako.
Lakini kuwa na mtandao wa watu pekee hautoshi kama hautawasiliana nao. Kuwasiliana na mtandao huo ni kuufanya uwe ‘active’ ili isionekane kama unawatafuta wakati ukiwa na shida tu. Aidha, unapaswa kujipima kwa kuangalia watu wangapi wanakufahamu wewe zaidi ya watu wangapi unaowafahamu. Kwa mfano: wewe unamfahamu Mkurugenzi wa kampuni ‘A’, Jiulize, je, yeye anakufahamu? Kama hakufahamu basi yeye sio sehemu ya mtandao wako.
Lakini pia, angalia mawasiliano yako ya siku, wangapi umeongea nao kuhusu wazo la biashara au kazi.
5. Kuwa mweli na Mwaminifu
Hii ni siri kubwa zaidi ya zote, japokuwa nimeiweka mwishoni kati ya hizi tano. Usipokuwa mwaminifu na mkweli huku unaona mambo yako yanaenda vizuri unapaswa kushtuka mapema. Wewe ni kama mtu anaevuka ng’ambo ya pili huku akilivunja daraja. Mwisho wa siku utajikuta unaporomoka kabla hujafika unakotakiwa kufika.
Uaminifu utaimarisha mtandao wako kwa hali ya juu zaidi na utatafutwa kwa kuwa wewe utakuwa sehemu ya sababu ya mafanikio ya watu wengine. Kwa mfano, angalia namba ulizonazo kwenye simu yako ya mkononi. Je, ukitaka kumpigia simu dereva taxi majira usiku au hata muda wa kawaida utatumia vigezo gani? Bila shaka uaminifu na ukweli vitatangulia zaidi.
Kuwa mwaminifu na mkweli kwa kila mtu utakayefanya nae kazi, biashara au hata wakati mnafanya mambo ya kawaida ya kijamii kunakupa nafasi ya kuwa chaguo la kwanza kwa watu wanapohitaji huduma, bidhaa au rasilimali ambayo unayo.
Ukifuata kwa uhakika haya matano huku ukimkumbuka Mungu wako kwa kila jambo utafanikiwa kweli na kubaki na amani ya moyo.
Amini katika kile unachoamini na kifanyie utafiti kujiridhisha kabla haujakubali kuyumbishwa kwa tamaa za haraka haraka ili uwe na sababu za kutosha za kukataa au kukubali jambo lolote.