Hakimu Atoa Neno Kesi ya Kutekwa Mo Dewji "Mshtakiwa Ahukimiwe Peke yake"


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetaka kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili dereva taxi, Mousa Twaleb kuendelea bila washtakiwa wengine ambao hawajakamatwa.

Twaleb  anakabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kumteka nyara mfanyabiashara maarufu Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Februari 4, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakamani hiyo, Huruma Shaidi wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Alieleza hayo baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

"Kwa nini mshtakiwa huyu asishtakiwe peke yake ili upelelezi wa kesi ukamilike  kwa wakati kuliko kuendelea kusubiri washtakiwa wengine ambao bado hawajakamatwa?”

"Hapa upelelezi unachelewa kukamilika kutokana na washtakiwa wengine ambao bado hawajakamatwa. Kwa nini asishtakiwe yeye ili kesi iendelee halafu hao wengine wakikamatwa watakuja kuunganishwa naye, au nyie mnasemaje upande wa mashtaka,"  amehoji hakimu huyo.

Hakimu Shaidi baada ya kutoa maelezo hayo, wakili wa upande wa mashtaka, Tulli Helela amedai maelezo hayo ameyapokea na atayapeleka kwa bosi wake kwa ajili ya uamuzi.

Awali, Wakili Helela alieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja ya upande wa mashtaka, ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 18, 2020.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad