Ifahamu njia mpya ya kuzika mwili ambayo ni rafiki kwa mazingira


Kampuni moja ya Marekani imetoa taarifa za kina kuhusu namna ya kuzika mtu kwa njia ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Utafiti wa majaribio ulifanyiwa maiti za watu walitoa idhini zao kabla ya wao kufa, umeonesha kwamba tishu laini mwilini huvunjika vunjika kwa njia salama na kuoza kabisa baada ya siku 30 tu.

Kampuni hiyo, inatumia njia za kufanya mwili uoze na kudai kwamba mchakato wanaotumia unazuia kaboni zaidi ya tani moja ikilinganishwa na njia zingine zinazotumika kama vile kuchoma mwili au kuuzika kwa namna ya kitamaduni iliyozoeleka.

Aidha, kampuni hiyo imesema itatoa huduma ya kuzika mwili kwa njia mpya katika jimbo la Washington kuanzia Februari mwaka ujao.

Akizungumza na BBC, mwazilishi wa kampuni ya Recompose, Katrina Spade, amesema kwamba wasiwasi kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa yamekuwa kichocheo kikubwa cha ubunifu wa njia mpya ya kuzika mwili huku wengi wakionyesha shauku ya kutaka kupata huduma hiyo.

"Hadi kufikia sasa, watu 15,000 wametia saini kukubali njia hiyo mpya ya kuzika mwili kupitia kijarida chao cha habari.

Na bunge kuruhusu huduma hii kuanza kutolewa katika jimbo ambalo iliungwa mkono na wengi na kupitishwa kwa mara ya kwanza ilipowasilishwa," amesema

"Njia hii imeendelea kuwa maarufu kwa haraka kwasababu ya uhitaji wa kukabiliana na mabadiliko hali ya hewa na kuelimisha jamii."

Bi Spade alizungumza na mimi baada ya matokeo ya utafiti wa kisayansi wa namna mpya ya kuzika mwili, ambayo kampuni ya Recompose inaitambua kama njia asilia ya kupunguza kemikali, ulikuwa unawasilishwa katika chama cha Marekani cha utafiti wa Kisayansi mjini Seattle.

"Kuna mambo yanayovutia katika utekelezaji wa njia hii mpya ya kuzika mwili,"alisema katika mahojiano ambayo amekuwa akifanyiwa tangu alipotangaza matokeo ya utafiti huo mwaka mmoja uliopita.

Ameniambia kwamba alipata wazo hilo miaka 13 iliyopita alipoanza kufikiria kuhusu kifo chake mwenyewe akiwa na miaka 30.

"Nitakapokufa, katika dunia hii ambayo imenilinda kwa kipindi cha maisha yangu yote, kwanini nisiiache katika hali nzuri kuliko nilivyoikuta?

"Si hoja tu iliyowazi lakini pia ina uzuri wake."

Bi Spade anaelezea tofauti iliyopo kati ya mwili kuzikwa namna ya kawaida na kwa namna mpya. Inaonesha kile kinachotokea punde tu mtu anapofariki. Na njia ya pili inajumuisha kuzika mwili.

Anadai kwamba upunguzaji kemikali kwa njia ya asili kwenye mwili baada ya kifo kutokea kunazuia tani 1.4 za kaboni kusambaa kwenye anga ikilinganishwa na mwili ambao umechomwa moto.

Pia anaamini kwamba njia mpya ni bora zaidi kuliko nama ya kawaida ya kuzika mwili ukijumuisha gharama za usafiri na sanduku la kuwekea maiti.

"Kwa wengi inaendana na namna wanavojaribu kuishi maisha yao. Wanataka kuchagua namna nzuri ya kuzika mwili inayoambatana na vile wanavoishi."

Mchakato huo unajumuisha kuweka mwili kwenye eneo lililofungwa lenye mbao, alfalfa na mabua. Kisha mwili huo unaanza kuzungushwa mduara taratibu ili kuruhusu bakteria kuozesha mwili kwa kuula.

Siku thelathini zitakazofuata kitakachokuwa ni mabaki tu ya mwili ambapo jamaa wanayachukua na kuyaweka kama mbolea ama kwenye mimea au miti na kadhalika.

Ingawa mchakato huo unaeleweka, imechukua miaka minne kwa utafiti wa kisanyansi kuusanifisha na kuifanya iwe njia bora. Bi Sapde alimtaka mwanasayansi wa masuala ya udongo Profesa Lynne Carpenter Boggs kutekeleza mchakato huo.

Mabaki ya wanyama kufanywa mbolea ni jamo la kawaida katika jimbo la Washington. Jukumu la Profesa Carpenter Boggs lilikuwa ni kutekeleza mchakato huo huo kwa mwanadamu na kuhakikisha kwamba ni salama kwa mazingira.

Alifanya majaribio na watu sita waliojitolea kushiriki kwenye utafiti na kutoa idhini zao kabla ya wao kufa.

Aliniarifu kwamba kazi hiyo ilikuwa yenye kuibua hisia kali kwake na timu nzima.

"Kila wakati tulikuwa tunajuliana hali. Mwili wangu ulikuwa na hisia tofauti, siku za kwanza sikuweza kupata usingizi vizuri usiku, sikuwa na hisi njaa - ilikuwa ni jambo lenye kuhuzunisha na kusononesha."

Profesa Carpenter Boggs alibaini kwamba mwili ambao ulizikwa kwa kutumia njia mpya, joto lake lilifikia nyuzijoto 55 ndani ya kipind fulani.

"Tuna uhakika kwamba viini vinavyosababisha magonjwa kwa kiasi kikubwa viliharibiwa na dawa kwasababu ya kiwango cha juu cha joto kilichofikiwa."

Kuzika miili kwa njia hii mpya itaanza kuwa biashara baadae mwaka huu. Yeyote yule anaweza kushiriki katika mchakato huu lakini ni halali tu katika jimbo la Washington.

Kwa sasa pia jimbo la Colorado linafikiria kuhalalisha njia hii mpya ya kuzika miili ya walioaga dunia ambayo kwa kiasi kikubwa ni njia asili ya kupunguza kemikali. Bi Spade anaamini kwamba ni muda tu lakini mbinu hii itasambaa katika maeneo mengine ya Marekani na kwengineko.

"Ni matumaini yetu kwamba majimbo mengine pia yatapitisha njia hii punde tu itakaposhika kasi katika jimbo la Washington.

Wengi kutoka Uingereza na maeneo mengine duniani wameonesha shauku na tuna matumaini ya kufungua matawi mengine ya ofisi zetu kwengineko tukiweza."
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad