Watu wawili walioambukizwa virusi vya Corona nchini Iran wamefariki, na kufikisha idadi ya waliofariki nchini humo kuwa watu 16, maafisa wamesema leo, wakati Wairan wakiwa na hofu kuwa huenda viongozi hawatilii maanani kiwango cha maambukizi.
Iran ina idadi kubwa ya vifo kutokana na virusi vya Corona nje ya China, ambako virusi hivyo vilianzia mwishoni mwa mwaka 2019.
Miongoni mwa wale walioambukizwa ni pamoja na naibu waziri wa afya, ambaye alipatikana kuwa ameambukizwa virusi hivyo vya Corona.
Maambukizi mapya ya virusi vya Corona vimethibitishwa leo nchini Italia pamoja na Austria, Croatia na nchini Uhispania, masaa kadhaa kabla ya mkutano wa mawaziri wa afya wa Umoja wa Ulaya unaofanyika leo.
Waziri mkuu wa Croatia Andrej Plenkovic amesema nchi hiyo ina mgonjwa mmoja.Idadi jumla ya wagonjwa nchini Italia imepanda hadi watu 283, ikiwa ni ongezeko la watu 54 kuanzia jana jioni.